WITO wa Rais Jakaya Kikwete wa kutaka wananchi wajitokeze kutaja
majina ya wahalifu nchini, umepata mwitikio mpya, safari hii watu kadhaa
wakijitokeza kutaja majina ya vigogo wanaoongoza kwa biashara ya dawa
za kulevya nchini.
Majina hayo yako katika barua iliyoandikwa na wananchi 15 kwenda kwa
Rais Kikwete, ambamo wanadai kwamba walikuwa wakitumiwa na vigogo hao
kufanya biashara hiyo, lakini sasa wameamua kuachana nayo. Barua hiyo
iliandikwa Septemba 8, mwaka huu na wahusika wanadai wamekwisha
kuiwasilisha Ikulu.
Kwa mujibu wa barua hiyo, majina 58 yameorodheshwa yakiwa katika
makundi matatu makubwa, la kwanza likiwa ni waagizaji wakubwa wa dawa
hizo; la pili niwafadhili ambao majina yao hutumika kusafirisha dawa
hizo; na la tatu ni wauzaji walioko Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Mbeya
na Zanzibar.
Katika orodha ya waandishi wa barua hiyo wanaodai kusukumwa na
uzalendo na uchungu kwa nchi yao, yamo majina ya wafanyabiashara maarufu
nchini na wanasiasa,wakuu wa taasisi nyeti, baadhi ya viongozi wa dini
na maafisa wa juu serikalini.
Kundi la kwanza lina majina 12, miongoni mwao ni wafanyabiashara
maarufu katika miji ya Dar es Salaam, Morogoro, Zanzibar, Arusha na
Bagamoyo na baadhi ya viongozi wa dini wa madhehebu fulani.
Kundi hili linadaiwa kuwa linaingiza dawa za kulevya kwa njia
mbalimbali zikiwamo, kutumia mipira ya kondomu, majokofu, vifaa vya
hospitali, meli na marobota ya mitumba.
Katika kundi la pili kuna watu 19, miongoni mwao wamo wanasiasa
wakubwa nchini wakiongoza kundi hili, kutoka taasisi ya fedha nchini na
wafanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam na Zanzibar.
Kundi la tatu lina majina 27, ambao si ya watu wenye majina makubwa,
lakini ndio wanaotumika kusambaza mitaani kwa watumiaji wa dawa za
kulevya.
Mbali ya kushiriki katika kusambaza dawa za kulevya, kundi hili pia
lina baadhi ya majina ya watu waliotajwa kushiriki katika kuingiza
silaha nzito zinazotumika kwa ajili ya ujambazi kutoka nchi jirani.
Ufukwe wa Pwani ya Bahari ya Hindi eneo la Muhoro wilayani Rufiji
inaelezwa kuwa linatumika kuingizia silaha hizo kutoka nchi jirani
pamoja na dawa za kulevya chini ya ufadhili wa mmoja wa wanasiasa
nchini.
Uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K. Nyerere unatajwa kuwa unatumiwa na
watu hawa kuingiza dawa hizo nchini kutokea nchi za nje, huku baadhi ya
maafisa wa polisi watatu wakitajwa kuwa ndio wanaotoa ulinzi kwa watu
wanaopitisha dawa hizo.
Nyumba ya afisa wa juu mstaafu katika idara nyeti iliyopo jijini Dar
es Salaam inatajwa kuwa inatumika katika kuhifadhi vijana wanaoingiza
dawa za kulevya nchini, huku nyumba ya mfanyabiashara mmoja iliyopo
Mikocheni jijini Dar es Salaam ikitajwa kuwa ndiyo inayotumika kama
kituo cha kutolea pipi tumboni kwa vijana wanaotumika kuingiza dawa hizo
kutoka nje ya nchi.
Vile vile, katika kundi hili mwanamke mmoja anayefanya kazi katika
taasisi moja ya fedha anatajwa kuwa anashiriki katika kuhujumu uchumi wa
nchi kwa kusafirisha kwenda nje fedha nyingi za kigeni akitumiwa na
mfanyabiashara mmoja maarufu wa dawa za kulevya nchini.
Mipaka ya Tunduma mkoani Mbeya, Horohoro mkoani Kilimanjaro na
Namanga mkoani Arusha, nayo imetajwa kuwa inatumika kupitisha dawa za
kulevya kwa kutumia mabasi na magari mengine. Kuna kampuni mbili za
mabasi nchini zinazotajwa kuongoza kutumika katika usafirishaji.
Barua hiyo ya kurasa 10, pia inamtaja mwanamke mmoja ambaye anatumika
kupitisha dawa za kulevya uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kuwa ni
sugu; aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 35 jela kwa kosa la
kupatikana na dawa za kulevya, lakini hivi sasa yupo mitaani kifungo
chake akitumikia mtu mwingine.
Alipoulizwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, alisema hajapata barua hiyo na kwamba
atalizungumzia baada ya kuipata.
Naye Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, alisema hana taarifa
za kuwako kwa barua hiyo. Hata hivyo, alisema kuna tume ya dawa za
kulevya iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inayoshughulikia
zaidi suala hilo.
Alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi za kukamata watu
wanaojihusisha na dawa hizo na kwamba mikakati mingine ya kupambana na
watumiaji inafanywa na tume hiyo.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Kikwete aliagiza Jeshi la Polisi
liongezewe uwezo wa kupambana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na kuwahamisha
vituo vya kazi askari waliokaa kituo kimoja kwa muda mrefu.
Pia alilitaka Jeshi hilo lijisafishe lenyewe kutokana na madai kwamba polisi wanahusika na baadhi ya matukio ya uhalifu nchini.
Rais alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa zozote za uhalifu, na
wanaojua waliko majambazi wazipeleke taarifa hizo kwake kama wanaogopa
kuzipeleka polisi.
Katika kuitikia wito huo, wananchi kadhaa waliandika barua
iliyoorodhesha majina ya polisi 20, wakiwamo baadhi ya makamanda wa
polisi wa mikoa na kuikabidhi kwa Waziri wa Usalama wa Rais, Bakari
Mwapachu.
Tangu wakati huo, mabadiliko makubwa yameshuhudiwa yakifanywa kwenye
jeshi hilo, hata hivyo hii ni mara ya kwanza kwa watu kujitolea kuandika
barua yenye majina na maelezo ya kina kama hii kuhusu biashara ya
kulevya na kuipeleka kwa Rais.
SOURCE: Mwananchi
إرسال تعليق