Na Saleh Ally
Yanga damu aliyevuliwa viatu na mashabiki wa Simba SC
MMOJA wa wanasiasa machachari nchini ni Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), amekuwa akitajwa
karibu kila sehemu yanapozungumziwa masuala mbalimbali yanayohusiana na
siasa hapa nchini kutokana na umaarufu alionao.
Lakini Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amekuwa akizungumziwa au
kuhusishwa karibu kila sehemu inayohusisha vurugu, mfano bungeni na
amekuwa na sifa ya kutokuwa na woga hata kidogo.
Kwa sasa ni kati ya wanasiasa walio msitari wa mbele kupambana katika
sakata linaloendelea dhidi ya mbunge mwingine kijana na machachari,
Zitto Kabwe. Hayo yote, yanabaki kuwa yao lakini tukirudi kwenye
michezo, Lissu ana mengi ya kusimulia.
Kuna watu ambao hawaamini kama wanasiasa wanaweza kuwa na muda wa kufanya mazoezi au kuvutiwa na michezo mbalimbali.
Pamoja na pilika za kisiasa na mapambano ya kila siku, Lissu anasema
anavutiwa na michezo mbalimbali lakini soka ndiyo namba moja.
Bila ya kujali rangi za njano na kijani, anasema kwa hapa nyumbani yeye
ni shabiki wa kikosi cha mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, ambao
wameweka kambi nchini Uturuki kujiandaa na mzunguko wa lala salama wa
ligi hiyo pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Lissu ana zaidi ya miaka kumi hajawahi kugusa uwanjani
kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara zikipigwa kwenye uwanja wowote ule na
zaidi amekuwa akilazimika kuangalia kwenye runinga.
Si kwamba hana muda au hana uwezo wa kufika uwanjani, badala yake
kinachosababisha asifike uwanjani ni mashabiki wa Simba. Unaweza
kujiuliza wao wanamzuia vipi kufika uwanjani wakati anashangilia timu
nyingine?
“Mimi napenda sana mpira, timu yangu ni Yanga. Ila siku hizi sipendi
kabisa kwenda uwanjani kuangalia mechi, napenda kuangalia kwenye runinga
tu,” anasema Lissu.
“Mara nyingi naangalia nyumbani kwenye runinga au hata baa, nakaa
naangalia na si kwenda uwanjani,” anaongeza. Alipoulizwa sababu ya
kutokwenda uwanjani wakati ana uwezo wa kufanya hivyo, alisema:
“Nakumbuka mwaka 1993 nilikwenda uwanjani wakati Simba ilipocheza na
Stella (ya Ivory Coast), siwezi kuisahau siku hiyo namna mashabiki wa
Simba walivyonifanya, sijasahau hadi leo.”
Siku hiyo Simba ilicheza mechi ya fainali ya Kombe la Caf dhidi ya
Stella Abidjan ya Ivory Coast. Wakati mashabiki wengi walijitokeza
Uwanja wa Taifa, Temeke jijini Dar es Salaam wakiamini Wekundu wa
Msimbazi wangebeba kombe hilo, mambo yalikuwa tofauti.
Wengi waliamini Simba ingeshinda kutokana na mambo mawili, kwanza sare
ya bila kufungana waliyoipata ugenini mjini Abidjan. Lakini pia ulikuwa
ni ubora wa kikosi cha Simba kilichokuwa na wachezaji kama Mohammed
Mwameja, George Masatu, Ramadhani Lenny, Hussein Marsha, Edward Chumila,
Malota Soma na wengine kibao.
Mwisho wa yote Simba ililala kwa mabao 2-0, huku aliyefunga mabao yote,
Boli Zozo, akijijengea jina hapa nchini. Hasira za mashabiki wa Simba
zilikuwa juu, walikuwa wakorofi, walikuwa wakiwapiga watu walioamini
walikuwa wana furaha wao kupoteza mchezo huo. Lakini vibaka nao
wakatumia nafasi hiyo kuchukua riziki haramu.
Lissu anasema akiwa anatokea uwanjani, alikutana na tafrani kama hilo
ambalo liliwakuta wengi siku hiyo na wamekuwa wakiendelea kusimulia.
“Nakumbuka nilikuwa nimefika eneo la Kidongo Chekundu, walitokea
mashabiki tulioambiwa ni wa Simba, walinizunguka na kunibeba juujuu.
Wakati wananishusha chini sikuwa na viatu wala pochi, wangeweza kunivua
hata suruali.
“Wakati bado nashangaa, dereva taxi mmoja ndiye alinisaidia kunipeleka
Chuo Kikuu, wakati huo nilikuwa bado mwanafunzi. Tangu siku hiyo
sijawahi kurudi uwanjani,” anasema.
Kuhusiana na mazoezi, Lissu anasema amekuwa akishiriki ingawa si kwa
kiasi kikubwa: “Mazoezi ni kitu kizuri sana, inabidi nishiriki kwa ajili
ya kujiweka vizuri tu.”
Kuhusiana na Chadema kushiriki katika michezo, Lissu anasema: “Kweli
michezo ni ajira, siwezi kusema tumefanya nini kama chama, lakini naweza
kusema katika hili vizuri tukaondoka katika kauli za uhamasishaji,
tumechoshwa.
“Usione tuko kimya, tumechoshwa na kauli hizo, sasa ni wakati wa vitendo
na kama tunataka tuwe taifa la michezo kama wenzetu Kenya wanavyofanya
vizuri kwenye Olimpiki au mataifa ya Afrika Magharibi na soka, basi
lazima tuwekeze kwa vijana na si maneno tu.
Post a Comment