Mzozo huko Sudani Kusini unafanya hali ya uchumi na usalama kuwa wa wasiwasi Afrika Mashariki

Wakenya ambao walikimbia mapigano huko Sudani Kusini wakiwasili Uwanja wa ndege wa Wilson huko Nairobi tarehe 3 Januari. [AFP]
Na Bosire Boniface, Nairobi

Mzozo unaoendelea huko Sudani Kusini unaathiri vibaya uchumi na usalama wa Kenya, na wachunguzi wanasema kutakuwa na mgawanyiko mkubwa kwa Afrika Mashariki kama mapigano hayatamalizika mapema.


"Vurugu za Sudani Kusini zinaibua wasiwasi mkubwa wakati tukitafuta ukuaji wa uchumi na muunganiko wa Afrika Mashariki," Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kenya kwa Mambo ya Nje Amina Mohammed aliiambia Sabahi. "Kenya tayari imeshaonja kero hizo. Ndiyo maana tunafanya kila linalowezekana ikiwa ni pamoja na jitihada za kusaidia kuhakikisha kwamba hali hiyo haiendelei."

Umwagaji damu huko Sudani Kusini ulianza tarehe 15 Desemba wakati mapigano yalipoanza kati ya vikundi vya wanajeshi wanaomuunga mkono rais Salva Kiir na wale wanamuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar.

Kikundi cha Kimataifa cha Migogoro kinakadiria kwamba karibia watu 10,000 wameshauawa katika mzozo huo, na kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Uratibu wa Masuala ya Ubinadamu (OCHA), watu wanaokadiriwa kufikia 413,000 wamekosa makazi ndani ya nchi wakati wakimbizi 74,300 wamekimbilia nchi jirani.

Jitihada za usuluhishi zinazolenga kufikia mkataba wa kukomesha mapigano zinaendelea huko Ethiopia chini ya msaada wa Mamlaka baina ya serikali kuhusu Maendeleo.

Katibu wa Masuala ya Mambo ya Nje wa Kenya alisema vurugu za Sudani Kusini zimeleta tatizo la kiuchumi kwa wawekezaji wa Kenya ambao walikuwa na nafasi katika taifa hilo linaloibua hofu. Wafanyabiashara na makampuni ya Kenya, hususani katika sekta ya mabenki na ujenzi, wamepiga hatua kubwa huko Sudani Kusini, alisema.

Mohammed pia alisema biashara za Wakenya zimeharibiwa na vurugu hizo. Aliongezea kwamba kama mzozo hautaisha hivi mapema, athari za kiuchumi zitasikika nchini Kenya, kwani maelfu ya raia ambao walipoteza fursa za kazi huko Sudani Kusini wanarejea nyumbani kutafuta fursa mpya zinazopatikana Kenya.

Kwa upande wa kanda, miradi ya pamoja ya uwekezaji kama vile Bandari ya Lamu - Sudani Kusini - Ethiopia (LAPSSET) na reli ya kawaida yenye geji itaathiriwa kama mzozo huko Sudani Kusini utaendelea, alisema Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kenya kwa Masuala ya Afrika Mashriki Phyllis Kandie.

Sudani Kusini pia ni kiungo muhimu kati ya kanda ya Afrika Mashariki na Afrika Kaskazini kwa kigezo cha biashara, Kandie aliiambia Sabahi.

"Mzozo huu unamaanisha kuhamishia fedha zote na uangalifu kutoka kwenye miradi muhimu. Kama kanda tungetaka twende pamoja katika miradi muhimu, lakini ni suala nyeti la mkono mmoja kupata jeraha na mwili wote kuhisi maumivu," alisema.

Kandie aliongezea kwamba mzozo wa Sudani Kusini umetokea wakati ambao hususani nchi za Afrika Mashariki zipo katika kazi ngumu ya kupeleka askari katika nchi nyingine kama vile Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Somalia.

"Amani ni muhimu katika miradi yote inayotekelezwa na nchi za Afrika Mashariki ama kwa nchi binafsi au kwa pamoja. Pasipo hilo malengo yetu ya maendeleo yatabadilishwa," alisema.

Usalama wajihusisha na wakimbizi
Kenya pia inazingatia uwezekano wa uingizaji kwa wingi wakimbizi kutoka Sudani Kusini, ambao utazidisha kupunguza uwezo wa nchi. Tayari kuna wakimbizi zaidi ya 500,000 nchini Kenya, wakiwemo Wasomali wengi, Waethiopia na Wakongo.

Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kenya David Kimaiyo aliiambia Sabahi kwamba wakimbizi wanaweza kuleta changamoto ya usalama kwa nchi kwa kuwa inapambana na magenge na makundi ya uhalifu wa kupangwa. "Hatuna tatizo la kuwahifadhi wakimbizi, bali ni watu wahalifu ambao watajifanya kuwa ni wakimbizi," Kimaiyo alisema.

Alionyesha wasiwasi wake kwamba mgogoro unaweza kutokea kiurahisi na Wasudani wa Kusini wanaoishi kambi ya wakimbizi ya Kakuma na maeneo ya mjini, na kwamba uongezekaji wa vurugu pia unaweza kusababisha kutokuwa na usalama katika mpaka wa Kenya na Sudani Kusini.

"Kimsingi, kutokuwa na sheria na utulivu na majirani zetu wa karibu kutasababisha kujipenyeza kwa silaha haramu nchini Kenya. Hili linaweza kusababisha mfumuko mkubwa wa uhalifu kama vile uvamizi wa ng'ombe na uundwaji wa makundi hatari ya uhalifu," alisema.

Wakati huo huo, alisema usalama umeimarishwa katika mpaka wa pamoja ili kuwachuja mamia ya wakimbizi wanaokimbia mapigano.

Kuwaondoa Wakenya
Kuna Wakenya 12,000 walioandikishwa rasmi kama wanaishi na kufanya kazi Sudani Kusini, lakini "serikali haikushangazwa kujua kwamba wengine zaidi ya 20,000 hawakuandikishwa [ubalozini] wa Kenya," Waziri wa Mambo ya Nje Amina Mohammed alisema.

Alielezea idadi ya Wakenya wasioandikishwa huko Sudani Kusini ni matokeo ya kutoelewa kwa "raia wetu' kuhusiana na majukumu ya kazi za [kidiplomasia]".

Mohammed aliongeza kwamba wakati wa kuwaondoa raia wa Kenya, serikali ilipata matatizo katika kujua hasa ni wapi walipo baadhi ya watu hao wasioandikishwa. Serikali ya Kenya imesaidia kuwaondoa watu 3,000 hadi sasa, lakini mapigano yamesababisha vifo vya raia wa Kenya wapatao wanne.

Waliorejea tayari wanahisi kupoteza uelekeo kwa kuwa wabadilishaji wa fedha za kigeni wa Kenya wanakataa kuikubali fedha ya Sudani Kusini.

Hassan Abdi Ali, mwenye miaka 46, Mkenya anayeendesha lori la usafirishaji Sudani Kusini, aliiambia Sabahi hakuweza kubadilisha paundi 50,000 za Sudani Kusini alizorudi nazo.

"Katika kila duka la kubadilishia fedha za kigeni nililokwenda, ikiwemo benki, nimekataliwa," alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post