![]() |
| Wakenya ambao walikimbia mapigano huko Sudani Kusini wakiwasili Uwanja wa ndege wa Wilson huko Nairobi tarehe 3 Januari. [AFP] |
Na Bosire Boniface, Nairobi
Mzozo unaoendelea huko Sudani Kusini unaathiri vibaya uchumi na usalama
wa Kenya, na wachunguzi wanasema kutakuwa na mgawanyiko mkubwa kwa
Afrika Mashariki kama mapigano hayatamalizika mapema.
"Vurugu za Sudani Kusini zinaibua wasiwasi mkubwa wakati tukitafuta
ukuaji wa uchumi na muunganiko wa Afrika Mashariki," Katibu wa Baraza la
Mawaziri la Kenya kwa Mambo ya Nje Amina Mohammed aliiambia Sabahi.
"Kenya tayari imeshaonja kero hizo. Ndiyo maana tunafanya kila
linalowezekana ikiwa ni pamoja na jitihada za kusaidia kuhakikisha
kwamba hali hiyo haiendelei."
Umwagaji damu huko Sudani Kusini ulianza tarehe 15 Desemba wakati
mapigano yalipoanza kati ya vikundi vya wanajeshi wanaomuunga mkono rais
Salva Kiir na wale wanamuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais Riek
Machar.
Kikundi cha Kimataifa cha Migogoro kinakadiria kwamba karibia watu
10,000 wameshauawa katika mzozo huo, na kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa
Mataifa kwa ajili ya Uratibu wa Masuala ya Ubinadamu (OCHA), watu
wanaokadiriwa kufikia 413,000 wamekosa makazi ndani ya nchi wakati
wakimbizi 74,300 wamekimbilia nchi jirani.
Jitihada za usuluhishi zinazolenga kufikia mkataba wa kukomesha mapigano
zinaendelea huko Ethiopia chini ya msaada wa Mamlaka baina ya serikali
kuhusu Maendeleo.
Katibu wa Masuala ya Mambo ya Nje wa Kenya alisema vurugu za Sudani
Kusini zimeleta tatizo la kiuchumi kwa wawekezaji wa Kenya ambao
walikuwa na nafasi katika taifa hilo linaloibua hofu. Wafanyabiashara na
makampuni ya Kenya, hususani katika sekta ya mabenki na ujenzi,
wamepiga hatua kubwa huko Sudani Kusini, alisema.
Mohammed pia alisema biashara za Wakenya zimeharibiwa na vurugu hizo.
Aliongezea kwamba kama mzozo hautaisha hivi mapema, athari za kiuchumi
zitasikika nchini Kenya, kwani maelfu ya raia ambao walipoteza fursa za
kazi huko Sudani Kusini wanarejea nyumbani kutafuta fursa mpya
zinazopatikana Kenya.
Kwa upande wa kanda, miradi ya pamoja ya uwekezaji kama vile Bandari ya
Lamu - Sudani Kusini - Ethiopia (LAPSSET) na reli ya kawaida yenye geji
itaathiriwa kama mzozo huko Sudani Kusini utaendelea, alisema Katibu wa
Baraza la Mawaziri la Kenya kwa Masuala ya Afrika Mashriki Phyllis
Kandie.
Sudani Kusini pia ni kiungo muhimu kati ya kanda ya Afrika Mashariki na
Afrika Kaskazini kwa kigezo cha biashara, Kandie aliiambia Sabahi.
"Mzozo huu unamaanisha kuhamishia fedha zote na uangalifu kutoka kwenye
miradi muhimu. Kama kanda tungetaka twende pamoja katika miradi muhimu,
lakini ni suala nyeti la mkono mmoja kupata jeraha na mwili wote kuhisi
maumivu," alisema.
Kandie aliongezea kwamba mzozo wa Sudani Kusini umetokea wakati ambao
hususani nchi za Afrika Mashariki zipo katika kazi ngumu ya kupeleka
askari katika nchi nyingine kama vile Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na
Somalia.
"Amani ni muhimu katika miradi yote inayotekelezwa na nchi za Afrika
Mashariki ama kwa nchi binafsi au kwa pamoja. Pasipo hilo malengo yetu
ya maendeleo yatabadilishwa," alisema.
Usalama wajihusisha na wakimbizi
Kenya pia inazingatia uwezekano wa uingizaji kwa wingi wakimbizi kutoka
Sudani Kusini, ambao utazidisha kupunguza uwezo wa nchi. Tayari kuna
wakimbizi zaidi ya 500,000 nchini Kenya, wakiwemo Wasomali wengi,
Waethiopia na Wakongo.
Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kenya David Kimaiyo aliiambia Sabahi
kwamba wakimbizi wanaweza kuleta changamoto ya usalama kwa nchi kwa kuwa
inapambana na magenge na makundi ya uhalifu wa kupangwa. "Hatuna tatizo
la kuwahifadhi wakimbizi, bali ni watu wahalifu ambao watajifanya kuwa
ni wakimbizi," Kimaiyo alisema.
Alionyesha wasiwasi wake kwamba mgogoro unaweza kutokea kiurahisi na
Wasudani wa Kusini wanaoishi kambi ya wakimbizi ya Kakuma na maeneo ya
mjini, na kwamba uongezekaji wa vurugu pia unaweza kusababisha kutokuwa
na usalama katika mpaka wa Kenya na Sudani Kusini.
"Kimsingi, kutokuwa na sheria na utulivu na majirani zetu wa karibu
kutasababisha kujipenyeza kwa silaha haramu nchini Kenya. Hili linaweza
kusababisha mfumuko mkubwa wa uhalifu kama vile uvamizi wa ng'ombe na
uundwaji wa makundi hatari ya uhalifu," alisema.
Wakati huo huo, alisema usalama umeimarishwa katika mpaka wa pamoja ili kuwachuja mamia ya wakimbizi wanaokimbia mapigano.
Kuwaondoa Wakenya
Kuna Wakenya 12,000 walioandikishwa rasmi kama wanaishi na kufanya kazi
Sudani Kusini, lakini "serikali haikushangazwa kujua kwamba wengine
zaidi ya 20,000 hawakuandikishwa [ubalozini] wa Kenya," Waziri wa Mambo
ya Nje Amina Mohammed alisema.
Alielezea idadi ya Wakenya wasioandikishwa huko Sudani Kusini ni matokeo
ya kutoelewa kwa "raia wetu' kuhusiana na majukumu ya kazi za
[kidiplomasia]".
Mohammed aliongeza kwamba wakati wa kuwaondoa raia wa Kenya, serikali
ilipata matatizo katika kujua hasa ni wapi walipo baadhi ya watu hao
wasioandikishwa. Serikali ya Kenya imesaidia kuwaondoa watu 3,000 hadi
sasa, lakini mapigano yamesababisha vifo vya raia wa Kenya wapatao
wanne.
Waliorejea tayari wanahisi kupoteza uelekeo kwa kuwa wabadilishaji wa
fedha za kigeni wa Kenya wanakataa kuikubali fedha ya Sudani Kusini.
Hassan Abdi Ali, mwenye miaka 46, Mkenya anayeendesha lori la
usafirishaji Sudani Kusini, aliiambia Sabahi hakuweza kubadilisha paundi
50,000 za Sudani Kusini alizorudi nazo.
"Katika kila duka la kubadilishia fedha za kigeni nililokwenda, ikiwemo benki, nimekataliwa," alisema.
Source: sabahionline.com

إرسال تعليق