Bodi
ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji
(EWURA) imepitisha maombi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) kuhusu kanuni za tozo za huduma ya kuchakata na kusafirisha gesi
asilia.
Pamoja
na maamuzi hayo pia EWURA imewataka TPDC kutimiza masharti ya
kuzingatia kanuni za ushindani kama zilivyoainishwa katika sheria ya
manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na kuiarifu Ewura kila watakapofanya
manunuzi ya thamani yanayozidi dola za Marekani milioni tano.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini, Mkurugenzi Mkuu EWURA, Felix Ngamlagosi
alisema TPDC iliiomba Ewura kuidhinisha vipengele vya kanuni ya
kurekebisha tozo za kuchakata na kusafirisha gesi asilia itumike kwa
miaka 20 hadi mwaka 2034, tozo kwa huduma ya kuchakata na kusafirisha
gesi asilia iwe katika dola za Marekani.
Pia
waliomba faida kwenye mtaji ya asilimia 18 na muundo wa mtaji wa
asilimia 50 mkopo na asilimia 50 fedha za TPDC na mwezi Septemba kila
mwaka wa tatu utakuwa ni mwezi ambao marekebisho ya tozo kwa miaka
mitatu inayofuata yatawasilishwa kwa EWURA.
Alisema
bodi ya EWURA ilijadili ombi la TPDC na kufikia maamuzi ya kipindi
kifupi cha miezi mitatu ambacho TPDC itakitumia kukamilisha ujenzi na
kuwasilisha gharama halisi ambayo EWURA iliyahoji.
Aliongeza
kuwa maamuzi yaliyotolewa na EWURA ni kanuni ya kukokotoa tozo za
kuchakata na kusafirisha gesi asilia iliyoombwa ilirekebishwe na
kupitishwa ili itumike kwa miaka 20 kuanzia mwezi Aprili mwaka huu na
kurekebishwa kila baada ya miaka mitano.
Pia
gharama za mradi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam zilizopitishwa ni sawa na dola za Marekani milioni
1,331,51 ambapo gharama hizi zitabaki hivyo hadi mwezi Juni hadi gharama
halisi za mradi zitakapojulikana na kufungwa.
Alisema
maamuzi mengine ni gharama za uendeshaji zitakuwa sawa na dola za
Marekani milioni 241.58 kwa mwaka na muundo wa mtaji kwa ajili ya mradi
wa bomba la gesi asilia Mtwara hadi Dar es Salaam litagharamiwa kwa
mkopo wa kiasi cha asilimia 75 na mtaji wa TPDC.
Aidha
mradi wa miundombinu ya bomba na mitambo ya kuchakata gesi asilia
utatekelezwa kipindi cha miaka 20 kutoka tarehe ya uzinduzi wake na
tozo ya kuchakata gesi italipwa kwa Shilingi ya Tanzania kwa kiasi sawa
na jumla ya dola za Marekani 2.14 kwa uniti ambapo tozo ya kuchakata
gesi itakuwa dola za Marekani 0.95 kwa uniti na tozo ya kusafirisha
gesi itakuwa dola za Marekani 1.19 kwa uniti.

Post a Comment