Kuna kila dalili kazi ya uzalishaji wa muziki wa Bongo Fleva itapotea au kupoteza thamani miaka michache ijayo.
Ni vigumu kusema hivyo na ukaeleweka na jamii ya
wasanii na maelfu ya mashabiki wao. Lakini huo ndiyo ukweli, iwapo hali
ya masilahi inayolegalega katika studio mbalimbali nchini haitaimarika.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya wazalishaji wa
muziki wa Bongo Fleva nchini wamekuwa wakilalamikia tabia ya mastaa wa
muziki huo kutumia fedha kidogo kurekodi nyimbo, huku wakitumia
mamilioni kurekodi video nje ya nchi.
Mzalishaji mkongwe nchini Master J hivi karibuni
alinukuliwa na tovuti ya Bongo 5 akilalamikia aina hiyo mpya ya
‘unyonyaji’. Master J alisema ni dhambi na hakuna kitu kinachouma kama
kumrekodia msanii wimbo kwa bei ndogo ya Sh200, 000 baadaye akaenda
kurekodi video yake kwa Sh25 milioni Afrika Kusini.
Kulalamika kwa ‘prodyuza’ huyo kumenifanya nipate
hofu juu ya hatima ya uzalishaji na ubora wa mziki huo siku zijazo.
Habari nyingine kuwa watayarishaji nchini ni maskini kuliko wasanii ni
ishara tosha kuwa kazi hiyo inapoteza thamani na imeingiliwa na mamluki.
Pia, inasikitisha kusikia Marco Chali amevunjika
moyo kutokana na ‘unyonyaji’ huo na ameacha kufanya kazi. Hii inazidi
kuleta wasiwasi katika tasnia ambayo imekuwa kitambulisho muhimu cha
Tanzania baada ya Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Zanzibar. Sote
tunafahamu kuwa hakuna Bongo Fleva au video ya wimbo pasina maprodyuza,
lakini kwa nini masilahi kidogo wakati wao ndiyo wakunga? Ili kufahamu
sababu za msingi lazima tuangalie asili na mfumo wa biashara ya Bongo
Fleva tangu miaka 1990.
Kuna tatizo kubwa la kimfumo wa biashara katika tasnia hiyo ambalo linaikumba pia tasnia ya filamu, Bongo Movie, kwa sasa.
Wakati Bongo Fleva inaanza miaka ya 1990 na
mwanzoni mwa 2000 kushika, ilikuwa ni shida kwa msanii kupata studio na
kurekodi wimbo wake. Mfumo wa biashara ulikuwa unatawaliwa na studio
chache tu kama Bongo Records, MJ Records, Sound crafters au kwa Mika
Mwamba.
Wazalishaji wa studio hizo akina Master J, P Funk,
Enrico na wengineo walisujudiwa na heshima yao ilionekana. Kibiashara
huo ndiyo ulikuwa muda muafaka wa kuujenga mfumo madhubuti wa biashara
ya Bongo Fleva.
Hata hivyo, Watayarishaji wengi walibaki wakifanya
huruma za kukuza wasanii chipukizi. Asilimia kubwa ya chipukizi na
mastaa walibaki katika lebo husika wakitengeneza albamu zao.
Mfumo huo ulitengeneza ‘watoto’ wa studio badala
ya wateja ambao wangelipa fedha inayotakiwa kwa huduma stahiki.
Tuliwaona akina Juma Nature, Marehemu Mangwair, Jay Moe wakikulia chini
ya Bongo Records na kuwa familia.
Mfumo wa aina hiyo ulitengeneza biashara ya ujamaa
zaidi badala ya ubepari. Biashara inalipa ukiifanya kiliberali na si
kwa kuoneana huruma na kubebana hata kama msanii kipaji kimeshuka au
kafilisika

Post a Comment