DUNIA
imekwisha jamani! Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya
Sekondari ya Mabibo, Dar, Irene Said (15) ametekwa, amebakwa na kuuawa
kikatili kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za
mwili huku ikidaiwa kuwa, kijana mmoja asiyejulikana alifika nyumbani
kwao, Kigogo Luhanga na kutaka kiroba na mtu mmoja waongozane akabebe
ndizi.
Akizungumzia tukio hilo la kusikitisha sana, mama mdogo wa marehemu, Doto Lucas alisema:
“Siku ya tukio ambayo ni Alhamisi iliyopita (Machi 12), kijana mmoja
ambaye hakuna aliyemfahamu alikuja hapa nyumbani na kumtaka mtu mmoja na
kiroba ili akachukue ndizi ambazo kuna mtu aliagiza ziletwe.
“Marehemu ndiye aliyekuwa karibu akijisomea baada ya kutoka shuleni. Mtu
mkubwa aliyekuwa nyumbani muda huo ni bibi wa marehemu ambaye ni mtu
mzima hivyo alimwambia Irene aongozane na mtu huyo akachukue mzigo
akijua uko jirani kwa mujibu wa mtu huyo.
“Baada ya muda, yule kijana alirudi akiwa peke yake na kusema anataka
chombo kingine cha kubebea kwa kuwa kile kiroba kilikuwa hakitoshi.“Bibi
mtu alimuonesha ndoo kwa vile hakukuwa na kiroba kingine, alipoitwaa na
kuondoka nayo ndiyo hakurudi yeye wala Irene.
“Baada ya kuona muda unayoyoma bibi wa marehemu alianza kupata wasiwasi.
Ndipo akatutaarifu kilichotokea nyumbani na sisi tukaanza kumsaka Irene
na kijana yule.”
KWA NINI WALIMWAMINI KIJANA HUYO?
“Sisi tuna makaka zetu wakubwa ambao wana kawaida ya kutuagizia mizigo
mbalimbali kwenye magari, kwa hiyo tuliamini ni wao. Lakini
tulipowapigia simu na kuwaeleza tukio hilo wote walikanusha kuwa si wao
na kushangaa.
“Kauli hiyo ilianza kututia shaka zaidi hivyo tulianza kuwasiliana na
ndugu na jamaa ambao wote waliishia kushangaa. Tukaenda kutoa taarifa
Kituo cha Polisi, Kigogo na kuanza msako wa kumsaka binti yetu pamoja na
mtuhumiwa.”
IRENE APATIKANA AKIWA AMEUAWA
Mwanamke huyo anaendelea kusimulia: “Kesho yake asubuhi (Ijumaa)
tukasikia kuna binti amekutwa ameuawa kinyama kwenye Bonde la Mto
Msimbazi, eneo la Sukita. Tulipatwa na mshituko, tukaenda na kuukuta
mwili, tulipoukagua tuligundua ni Irene.
“Alikuwa ameharibiwa vibaya. Sehemu za mwii alikuwa na damu, alichomwa
na kitu chenye ncha kali. Kwa vyovyote yule kijana alikuwa na wenzake,
walimteka huko mbele ya safari na kumbaka kabla ya kumuua. Inauma sana
jamani.”
Marehemu Irene ambaye katika mazishi yake wanafunzi wenzake walikuwa
wakilia sana, alizikwa Jumamosi iliyopita katika Makaburi ya Mburahati,
Dar.
Katika ibada hiyo, Katekista aliyesaidiana na paroko kuendesha ibada
hiyo aliyetajwa kwa jina moja la Henjewele aliwalaani vikali
walioshiriki kufanya unyama huo na kuwataka wafanye toba haraka
iwezekanavyo na kumrudia Mungu wao vinginevyo laana na moto wa milele
utawaangukia.
Mungu ailaze roho ya marehemu Irene mahali pema peponi- Amina.
Globalpublishers

Post a Comment