MKAKATI wa kumng’oa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson
Mukama, anayedaiwa kushindwa kukiendesha chama umeshika kasi, Tanzania
Daima Jumapili limebaini.
Mbali na Mukama, baadhi ya wabunge pia wanataka wenzao waliogoma
kuipitisha bajeti ya serikali nao kushughulikiwa kwa kukisaliti chama.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa baadhi ya wabunge na wanachama wanataka Mukama aachie ngazi au afukuzwe.
Duru za kisiasa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa matumaini
ya wanachama wengi wakiwamo vigogo wa chama hicho waliyokuwa nayo kwa
Mukama wakati anaingia madarakani yamefifia.
Katibu mkuu huyo aliyeingia madarakani kwa mbwembwe ndani ya CCM miaka
miwili iliyopita, anadaiwa kushindwa kabisa kukijenga chama kama
ilivyotarajiwa na badala yake ametengeneza mpasuko mkubwa ndani ya
chama.
CCM kwa sasa inakabiliwa na makundi makubwa mawili yenye wafuasi
wengi, moja ni lile linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete, ambaye amebaki na kundi linalojinadi kama wapinga ufisadi na
kundi jingine ni lile linaloongozwa na hasimu wake kisiasa, Edward
Lowassa, linalopingana na dhana ya kujivua gamba.
Mukama pia anadaiwa kushindwa kukiimarisha chama na kuruhusu wanachama
wengi kukihama chama hicho kwa kile kilichoelezwa kutoridhishwa na
mwenendo wa mambo ndani ya CCM.
Kiongozi huyo anabebeshwa lawama kuwa ameshindwa kusimamia dhana ya
kujivua gamba wakati yeye ndiye aliyeanzisha hoja hiyo kupitia tume
aliyoiongoza kufanya utafiti kubaini sababu za CCM kupata kura chache za
urais na kupokwa majimbo mengi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
“Unajua, Mukama ndiye aliyekuja na matokeo ya utafiti kwenye Kamati
Kuu na Halmashauri Kuu. Alibainisha sababu kadhaa za chama kushindwa,
lakini sababu kubwa tume yake ilibaini ni pamoja na chama kukosa mvuto
kutokana na baadhi ya makada wake, Edward Lowassa, Andrew Chenge na
Rostam Aziz kuhusishwa na ufisadi. Akaja na mapendekezo kwamba makada
hao wavuliwe nyadhifa zao.
“Leo ameshindwa kusimamia kile alichokiamini, badala yake chama
kimekuwa kikipiga vita ya maneno tu, mara kutoa siku 90, mara
tumeongeza, mara haijulikani. Matokeo yake tumezalisha makundi
yanayokitafuna chama,” alisema kada mmoja ambaye ni mjumbe wa NEC.
Kada huyo anasema kuwa baadhi ya makada wanaotuhumiwa kwa ufisadi
waliandaliwa barua za kutakiwa kuachia nyadhifa zao lakini hilo
lilishindikana kutokana na utendaji mbovu wa Mukama.
Makada wengine wanamlinganisha Katibu Mkuu Mukama na mtangulizi wake,
mzee Yusuf Makamba, kwamba licha ya kuwa na elimu ndogo ya darasani,
amemzidi Mukama kiutendaji.
Dalili za CCM kumchoka Mukama zimejionyesha hivi karibuni katika moja
ya vikao vya wabunge wa CCM ambapo baadhi walifikia hatua ya kusema
katibu mkuu wao amechoka kimawazo, bora aachie ngazi sasa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, mjini Dodoma zilisema wabunge walikuja juu wakati
walipokuwa wakijadili hali ya kisiasa ndani ya chama chao na kuwekeana
msimamo wa kuiunga mkono Bajeti ya mwaka 2012/2013.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM, aliliambia gazeti hili kuwa
katibu mkuu sasa hashirikishwi katika baadhi ya mambo baada ya kubaini
kuwa hana uwezo wa kukiimarisha chama.
“Angalia katika mikutano yote inayofanywa na chama kwa sasa hata ule
wa Jangwani ulikuwa na watu wengi, Mukama hakuwepo. Ingawa alikuwa nje
ya nchi, lakini hata kama angekuwapo, asingepata nafasi ya kuhutubia
kwani hana uwezo wa kuongea hadharani.
Kada mwingine wa CCM alimshmabulia Mukama kwa madai kuwa amekuwa akiropoka vitu ambavyo wakati mwingine hana utafiti navyo.
“ Mfano ni wakati wa kumuaga marehemu Bob Makani. Alitoa historia ya
ajabu kuhusu waasisi wa CHADEMA, matokeo yake, Freeman Mbowe, alimuumbua
pale alipotoa ufafanuzi kupinga kauli yake,” alisema.
Wabunge walioipinga bajeti kukiona
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa kuna mpango wa kutaka
kuwawajibisha baadhi ya wabunge waliokiuka msimamo wa pamoja wa wabunge
wa CCM juu ya kuipitisha bajeti.
Bajeti hiyo ya serikali iliyopitishwa Ijumaa wiki hii kwa kura 225 za
ndiyo huku kura 72 zikiikataa, kwa kupiga kura za hapana, zaidi ya
wabunge 54 hawakuhudhuria mkutano huo.
Kuna taarifa kuwa wabunge waliogoma kuhudhuria kikao hicho bila
taarifa na wengine waliokataa kuipitisha bajeti hiyo huenda wakakumbana
na mkono wa chama ambacho katika siku za hivi karibuni kimekuwa kikihaha
kujinusuru kutoka katika minyukano ya makundi yanayohasimiana.
Inasemekana baadhi ya wabunge wanataka wenzao wajadiliwe na
ikiwezekana wawajibishwe ili kujenga nidhamu chamani pamoja na kudumisha
uwajibikaji wa pamoja.
Wabunge hao wanatarajiwa kujadiliwa na kikao cha wabunge wa CCM
ambacho kinatarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo mara baada ya
kuwasilishwa kwa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wabunge wanaoonekana kuwasaliti wenzao ni Luhaga Mpina (Kisesa), Deo Filikunjombe (Ludewa) na Kangi Lugola (Mwibara)
cHANZO:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment