Tume ya Mabadiliko ya Katiba yatoa ratiba ya kazi ya kukusanya maoni


 Mwenyekiti wa Tume ya Mabadilo ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuanza kufanya mikutano na wananchi wa mikoa minane kuanzia siku ya Jumatatu, Julai 2, 2012 hadi Jumatatu, Julai 30, 2012 kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya
 
Mikoa hiyo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga. Katika mkoa wa Dodoma, Tume itaanza na Wilaya ya Bahi; Katika mkoa wa Kagera Tume itaanza na wilaya ya Biharamulo; Katika mkoa wa Manyara Tume itaanza na wilaya ya Mbulu na katika mkoa wa Pwani Tume itaanza na wilaya ya Mafia.
 
Kwa mkoa wa Shinyanga Tume itaanza na wilaya ya Kahama na kwa mkoa wa Tanga, Tume itaanza na Wilaya ya Lushoto. Kwa Zanzibar, Tume itaanza kukusanya maoni katika mkoa wa Kusini Unguja katika wilaya ya Kusini.
 
Taratibu zote za kuanza kazi zimekamilika zikiwemo kuandaa ratiba na kuisambaza katika mikoa na wilaya husika. Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika makundi saba. Kila kundi litafanya mikutano katika mkoa mmoja isipokuwa kundi moja litakalofanya mikutano katika mikoa miwili ya Kusini Unguja na Kusini pemba.
 
Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa uwazi, uhuru na utulivu.
 
Pamoja na kuwasilisha maoni kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume, wananchi pia wanaweza kuwasilisha maoni yao kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia anuani za zifuatazo:                     
i.                     Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makao Makuu, Mtaa wa Ohio, S.L.P 1681, DAR ES SALAAM, Simu: +255 22 2133425, Nukushi: +255 22 2133442; Au
ii.                    Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, S.L.P. 2775, Zanzibar, Simu: +255 224 2230768, Nukushi: +255 224 2230769

Post a Comment

Previous Post Next Post