Wakurugenzi wanane watemwa Tamisemi

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewavua madaraka wakurugenzi wanane, katika kushughulikia matatizo ya ufisadi na utendaji katika mamlaka za miji na wilaya nchini.

Katika hatua hizo, wakurugenzi watatu wamepumzishwa kazi wakisubiri uchunguzi, wakati wengine 11 wamepewa onyo kutokana na makosa mbalimbali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema jana mjini Dodoma kuwa katika kushughulikia matatizo ya ufujaji wa fedha za umma, kesi za wakurugenzi wawili zinaendelea mahakamani.

Mabadiliko hayo yamewezesha kuteuliwa kwa wakurugenzi wapya 14 na kwamba uteuzi wa wengine kwa ajili ya kuziba nafasi ambazo zimekuwa wazi kwa muda mrefu, bado unaendelea.Wakurugenzi 22 wamebadilishwa vituo vyao vya kazi.

“Wakurugenzi 14 wameteuliwa ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi, wakurugenzi wanane wamevuliwa madaraka na Waziri Mkuu, wengine watatu wamepumzishwa na uchunguzi unaendelea,” alisema Ghasia na kuongeza:

“Mabadiliko haya ni kwa ajili ya kuboresha utendaji wa kazi katika halmashauri zetu, pamoja na kuongeza nidhamu na uwajibikaji wa kazi kwa wakurugenzi ambao walikuwa si waadilifu katika kutekeleza majukumu yao.”

Alisema kwa waliovuliwa madaraka uchunguzi bado unaendelea na kwamba watakaobainika kuhusika na wizi wa fedha za umma watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Ghasia alisema uamuzi huo wa Serikali ulifanyika katika kipindi cha mwaka 2011/12 na kwamba baadhi ya waliopewa onyo, wamehamishwa vituo vyao vya kazi huku wengine wakiendelea kubaki katika vituo vyao vya awali.

Wapya walioteuliwa

Wakurugenzi wapya walioteuliwa na vituo vyao vya kazi kwenye mabano ni Jenifer Omollo (Mji wa Kibaha), Fidelica Myovela (Musoma), Khadija Maulid (Tabora) na Ibrahim Matovu (Muheza).

Wengine ni Idd Mshili (Mtwara), Julius Madiga (Morogoro), Kiyungi Mohamedi ambaye anakuwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Lucas Mweri ( Nanyumbu) na Miriam Mmbaga (Kigoma).

Wengine ni Mwamvua Mrindoko (Nachingwea), Pendo Malembeja (Kwimba), Pudenciana Kisaka (Ulanga), Ruben Mfune (Ruangwa) na Tatu Selemani ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha. Uteuzi huo ulianza rasmi Aprili 24 mwaka huu.

Waliovuliwa madaraka

Wakurugenzi waliovuliwa madaraka kutokana na makosa mbalimbali katika Halmashauri zao ukiwamo ubadhirifu wa fedha za umma ni Consolata Kamuhabwa (Karagwe), Ephraim Kalimalwendo (Kilosa) na Elly Jesse Mlaki (Babati).

Wengine ni Eustach Temu (Muheza), Jacob Kayange (Ngorongoro), Hamida Kikwega (Chato), Majuto Mbuguyu (Tanga) na Raphael Mbunda Halmashauri ya Manispaa ya Arusha.

Kwa upande wa waliopewa onyo kali Waziri Ghasia aliwataja kuwa ni Judetatheus Mboya (Newala), Lameck Masembejo (Masasi), Abdallah Njovu (Tandahimba) na Jane Mutagurwa (Shinyanga).

Wengine ni Silvia Siriwa (Sumbawanga), Kelvin Makonda (Bukombe),  Alfred Luanda (Ulanga), Fanuel Senge (Tabora), Maurice Sapanjo (Chunya) na Beatrice Msomisi wa Bahi.

Pia waziri huyo alibainisha kuwa katika mabadiliko hayo wakurugenzi watatu ambao ni Xavier Tiweselekwa wa Misungwi, Erica Mussica wa Sengerema na Theonas Nyamhanga wa Kishapu wamepumzishwa wakisubiri uchunguzi kukamilika.

Waliohamishwa vituo

Waliohamishwa vituo vyao vya kazi ni Elizabeth Kitundu kutoka Maswa kwenda Missenyi, Alfred Luanda kutoka Ulanga kwenda Kigoma/ Ujiji, Robert Kitimbo kutoka Mpwapwa kwenda Dodoma Manispaa, Shaban Ntarambe kutoka Kwimba kwenda Chato, Francis Namaumbo kutoka Masasi kwenda Mafia na Hilda Lauwo kutoka Ludewa kwenda Maswa.

Wengine ni Upendo Sanga kutoka Meatu kwenda Mbeya, Isaya Mngurumi kutoka Kisarawe kwenda Meatu, Lewis Kalinjuna kutoka Kigoma/ Ujiji kwenda Korogwe Mjini, Dominic Kweka kutoka Kigoma kwenda Babati, Lameck Masembejo kutoka Korogwe kwenda Kilosa na Azimina Mbilinyi kutoka Kibaha kwenda Kilombero.

Taarifa ya nyongeza iliyotolewa na Tamisemi pia inaonyesha kuwa Karaine Ole Kuney anatoka Musoma kwenda Ngorongoro, Mohamed Ngwalima kutoka Mtwara kwenda Kilolo, Gladys Dyamvunye kutoka Nanyumbu kwenda Masasi na Eden Munisi kutoka Morogoro kwenda Ludewa.

Wengine ni Anna Mwahalende kutoka Moshi kwenda Korogwe, Mathias Mwangu kutoka Ngara kwenda Manispaa ya Singida, Fanuel Senge kutoka Tabora kwenda Mpwapwa, Bosco Ndunguru kutoka Kilolo kwenda Karagwe, Christina Midelo kutoka Korogwe Mjini kwenda Iramba na
Yona Maki aliyehamishwa kutoka Manispaa ya Singida kwenda Kisarawe.

Taarifa hiyo ya nyongeza pia inawataja wakurugenzi ambao tayari wamefikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea kuwa ni Harold Senyagwa aliyekuwa Kyela na Rhoda Nsemwa aliyekuwa Bagamoyo

Post a Comment

Previous Post Next Post