SIMBA BINGWA NGAO YA JAMII, YAICHAPA AZAM GOLI 3 - 2

Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga (kulia) akimkabidhi Ngao ya Jamii, Nahodha wa Simba, Juma Kaseja. Pembeni yake ni beki Nassor Masoud 'Chollo' na kulia kabisa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani.
 Mashabiki wa timu ya Simba wakifuatilia mchezo kati ya timu hiyo na Azam FC, uliochezwa Uwanja wa Taifa kuwania Ngao ya Hisani, Dar es Salaam jioni hii.(PICHA NA KASSIM MBAROUK)
Ramadhan Chambo 'Redondo' wa Simba (kulia), akiwania mpira na Abdulhalim Humud wa Azam FC. 
 
 
SIMBA SC, inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager imetwaa Ngao ya Jamii, baada ya kuifunga Azam FC, mabao 3-2 jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar e s Salaam.
Shujaa wa Simba leo hii alikuwa ni kiungo Mwinyi Kazimoto aliyefunga bao la ushindi dakika ya 78 kwa shuti kali la mbali baada ya kumchungulia kipa wa Azam, Deo Munishi ‘Dida’ amekaaje.
Hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na kipre Herman Tchetche, wakimtungua kipa namba moja Tanzania, Juma Kaseja.
Bocco alitangulia kufunga dakika ya tano ya mchezo huo, baada ya kupigiwa kona fupi na Abdi Kassim ‘Babbi’, akatoa pasi kwa Abdulhalim Humud ambaye alimrudishia mfungaji huyo akafumua shuti kali la chini likajaa nyavuni pembezoni mwa lango kulia.
Bocco ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Simba SC leo, alimtoka Amir Maftah upande wa kulia wa Uwanja na kuingia ndani kabla ya kutoa krosi fupi kwa Kipre aliyemtungua Kaseja na kuipatia Azam bao la pili dakika ya 35.
Simba ilipata bao lake la kwanza dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza, baada ya kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, mfungaji Daniel Akuffo kwa penalti, baada ya Said Mourad kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha pili Simba walirudi na nguvu zaidi na kuamua kushambulia kwa mipira ya pembeni, ikiwatumia Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi ambao walikuwa wakibadilishana reli. 

Post a Comment

Previous Post Next Post