Na Majid Ahmed, Mogadishu
Jeshi la Somalia limeanzisha mpango mpya wa usalama mjini Mogadishu kwa
msaada wa Misheni ya Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM) ili kumaliza
mabaki ya al-Shabaab waliojificha jijini.
"Vitengo maalumu vya polisi vyenye dhamana ya kuzuia mashambulizi na
operesheni za kigaidi vinaanzisha mpango wa usalama ili kuisafisha
Mogadishu na al-Shabaab kwenye maficho yao," alisema Jenerali Abdullahi
Hassan Barise, mkuu wa uchunguzi wa jinai.
Katika usafishaji wa usalama chini ya mpango mpya, polisi hapo tarehe 10
Oktoba waliwabaini na kuwakamata mamia ya wanachama washukiwa wa
al-Shabaab. "Tuliwakamata watu 360 wakati wa operesheni za hivi karibuni
za usalama, lakini baada ya polisi na vikosi vya usalama kuwachunguza
washukiwa hawa, tuliweza kuthibitisha kwamba watu 62 miongoni mwao ni
wanachama wa al Shabaab wanaotakiwa na vikosi vya usalama wakati wale
wengine waliothibitishwa kuwa hawana hatia waliachiwa huru," Barise
alisema.
Maafisa wa polisi wanawake wakiangalia
wakati wa sherehe za ufunguzi wa mpango mpya wa mafunzo unafadhiliwa na
Misheni ya Umoja wa Afrika Somalia na Jeshi la Polisi la Somalia hapo
tarehe 15 Oktoba. [Na Tobin Jones/AFP]
"Polisi pia waligundua kiwango kikubwa cha silaha, ikiwa ni pamoja
milipuko, mabomu ya mikono, vifaa vya milipuko na silaha za automatiki
zilizofichwa majumbani huko wilaya ya Hodan mjini Mogadishu kupitia
habari zilizotolewa na wakazi wa eneo hilo,'' alisema.
Katika mpango huo mpya, ni wanajeshi na vikosi vya polisi vitaruhusiwa
kumiliki na kubeba silaha mjini, isipokuwa kwa walinzi wachache wa
usalama wa binafsi ambao wamepewa ruhusa rasmi na serikali ya Somalia.
Barise aliutaka umma kushirikiana na vikosi vya usalama na kutoa habari
ili kusaidia usalama wa Mogadishu. "Tunawataka wakazi kuvisaidia vikosi
vya usalama ili kumaliza maficho ya magaidi ambao kinyume chake
wanaathiri hali ya usalama," alisema.
Kanali Ali
Abdirahman, mmoja wa maafisa wa Jeshi la Usalama la Somalia
anayeshughulikia operesheni katika wilaya ya Hodan, alisema kuwa baadhi
ya watu 62 waliokamatwa walikuwa sehemu ya magaidi ambao walikuwa
wamejificha katika maeneo ya makazi ya watu wakati wa mchana na kufanya
vitendo vya ugaidi nyakati za usiku.
"Tutafanya msako katika vitongoji, nyumba hadi nyumba, kutafuta silaha
ambazo hazina leseni au milipuko, hasa katika maeneo ambayo vikosi vya
usalama vinashutumu kuwa wanachama wa al-Shabaab wanajificha," aliiambia
Sabahi. "Operesheni hizi zitaendelea hadi wanachama wa al-Shabaab
watakapoangamizwa ndani ya jiji."
Doria za usalama usiku
Kepteni wa Polisi Mohamed Ibrahim alisema kuwa mpango mpya wa usalama unajumuisha doria za usalama nyakati za usiku.
"Vitengo maalumu vya polisi vinapelekwa katika makutano makubwa ya
barabara na doria inafanywa kwa muda wa masaa 24 kwa siku," aliiambia
Sabahi, na kuongeza kuwa vitengo vya polisi kutoka Misheni ya Umoja wa
Afrika Somalia vinashiriki katika operesheni hizo za usalama.
"Vikosi vya pamoja vya polisi vinafanya doria za usalama na uvamiaji
holela dhidi ya nyumba ambazo washukiwa wa al-Shabaab na wale ambao
wanapinga amani wanajificha," alisema.
Ibrahim alisema ingawaje al-Shabaab wameshindwa kijeshi, mabaki ya
kikundi na wapenzi wao bado wanajificha miongoni mwa wakazi na jamii za
kienyeji katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa serikali.
"Vikosi vya usalama viko katika tahadhari ya hali ya juu ili kujikinga
na watu wanaojificha ili wasijikusanye na kuendelea na operesheni zao za
uharibifu mjini Mogadishu," alisema. "Tutaendelea na operesheni hizi
mpaka mabaki ya watu hawa ambao wanapinga amani wanamalizwa mjini
Mogadishu na maeneo ya karibu. Hatutasita hadi jiji na miji mengine iko
salama na huru kutokana na wanachama wa al-Shabaab."
Uwekaji nambari kwenye nyumba na usajili wa wakazi wote
Mohamed Yusuf, msemaji wa meya wa jiji la Mogadishu, alisema kuwa mpango
mpya wa usalama pia ni pamoja na sensa ya vitongoji vya Mogadishu na
usajili wa wakazi wa jiji.
"Uwekaji nambari katika nyumba unafanywa katika wilaya tano: Hamar
Weyne, Hamar Jajab, Wabari, Shangani na Bondheere," aliiambia Sabahi, na
kuongeza kuwa kuweka nambari katika kila mtaa mjini Mogadishu
kutasaidia kuhakikisha na kukinga usalama na utulivu wa mji mkuu.
Yusuf pia alisema kuwa wamiliki wa majumba wanapaswa kuwasiliana na
vikosi vya usalama vinavyohusika kabla ya kukodisha nyumba zao kwa watu
wanatiliwa shaka ili kujikinga na mabaki ya al-Shabaab wanaojificha
katika majengo ya makazi ya watu.
Polisi wapiga marufuku magari yenye vioo vya giza
Askari wa trafiki pia wametoa amri ya kupigwa marufuku magari yenye vioo vya giza.
"Sheria hii ilitolewa ili vikosi vya usalama viweze kuwatambua abiria
waliomo ndani ya gari hizo," Omar Hassan, afisa wa polisi wa usalama
barabarani, aliiambia Sabahi, na kuongeza kuwa upigaji marufuku huo
hauwajumuishi maafisa wa serikali na wabunge.
"Katika tukio ambapo dereva atakamatwa anaendesha chombo chenye vioo vya
giza, tutamuamrisha kuondoa plastiki nyeusi kwenye madirisha ya magari
yao," alisema. "Ikiwa watajaribu kutotimiza hilo au kujaribu kuweka
plastiki nyeusi inayoganda kwenye magari yao, wataadhibiwa."
Post a Comment