Kauli ya rais Kikwete kuhusu makanisa kushambuliwa na Waislamu Mbagala

6 Kauli ya rais Kikwete kuhusu makanisa kushambuliwa na Waislamu Mbagala
Uharibifu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza kusikitishwa kwake na vitendo vya baadhi ya Waislamu, waliochukizwa na madai ya mtoto kukojolea na kutemea mate Msaafu, kuharibu na kuchoma moto makanisa katika vurugu walizofanya Mbagala. Zifuatazo ni baadhi ya nukuhu za alichosema rais Kikwete, baada ya kufanya ziara ya ghafla ya kuyatembelea makanisa yaliyoshambuliwa na kuharibiwa. “Jamani poleni sana…Nimekuja kuwapeni pole kwa tukio lililotokea. Ni mambo yanayosikitisha, yanayotia fedheha na yanayoleta aibu kwa Taifa la Tanzania.”
“Ni tukio linalotia doa undugu na urafiki baina ya Waislamu na Wakristo uliodumu nchini kwa miaka mingi sana nyuma. Ni kweli kwamba kijana aliyekojolea kitabu ya Kurani alifanya kosa, lakini kosa hilo lilikuwa tayari limedhibitiwa na vyombo vya kisheria.”
“Kitendo cha kushambulia makanisa ambayo pengine hata hayakumtuma na pengine hayamfahamu kabisa kijana yule ni cha fedheha, aibu na kinaleta masikitiko makubwa sana. Nimeambiwa tayari watu 122 wamekamatwa na 36 kati yao ni wale waliokuwa wamelizunguka kanisa, nataka niwahakikishie kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wote waliohusika.”
Tofauti na kawaida yake, ambapo huwa na nyuso ya furaha na ucheshi, Rais Kikwete aliwasili katika Kanisa la Kiinjili la Kirutheri (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jimbo la Kusini, Usharika wa Mbagala, akiwa mwenye nyuso ya huzuni na sauti yake ikidhihirisha masikitiko aliyokuwa nayo kuhusu tukio hilo.
Rais Kikwete alilakiwa kwa kilio na baadhi ya waumini waliokuwa wamekusanyika kanisani hapo. Rais aliwapa pole na kuwataka wawe watulivu na wenye moyo wa kutotaka kulipiza kisasi.
“Ombi langu ni kwa viongozi kukabili changamoto ya kufanya kazi katika mazingira magumu. Uamuzi wa watu kuvamia makanisa na kufanya uharibifu kama huu ni uamuzi wa makosa.”
“Sitarajii kama Kanisa linaweza kuwa na moyo wa kulipiza kisasi kwa tukio kama hili maana kisasi hakisaidii sana na badala yake tutazidi kuivuruga nchi yetu. Kitendo hiki kinaweza kujenga picha kwamba kuna ugomvi mkubwa sana baina ya Waislamu na Wakristo katika nchi yetu ya Tanzania, jambo ambalo si sahihi.”
“Nawahakikishia hakuna yoyote aliyehusika na tukio hili ambaye ataachwa. Hata wale watakaobainika walihusika kwa kutoa maelekezo au kwa kushinikiza wakiwa mahala popote watakamatwa na kushughulikiwa. Naomba tuviache vyombo vya sheria vifanye kazi yake. Ni jambo baya ni jambo la aibu na fedheha sana kwa nchi ya Tanzania,” alisema Rais Kikwete.
Katika ziara hiyo rais Kikwete alishuhudia kuchomwa moto na kuteketea kwa madhabahu ya kanisa hilo, kuvunjwa na kuibwa kwa fedha katika ofisi ya Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) kanisani hapo, kuharibiwa kwa madirisha, milango, vinanda na mali nyingine za kanisa hilo. Alipata nafasi pia ya kuyatembelea makanisa ya TAG na Anglikana ambayo pia yalishambuliwa na kuharibiwa katika tukio hilo.
Awali akimkaribisha Rais kuzungumza na waumini, Askofu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jimbo la Kusini, George Fupe, aliwataka waumini kuwa watulivu hasa baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Alex Malasusa kuwataka kuvaa nyoyo za uvumilivu na subira kutokana na tukio hilo.
Chanzo: ziro99.blogspot.com

Post a Comment

Previous Post Next Post