MASHINDANO YA MITUMBWI YAZINDULIWA


Meneja wa Bia ya Balimi, Edith Bebwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mashindano ya mitumbwi

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Balimi Extra Lager, jana imezindua rasmi Mashindano ya Mitumbwi Kanda ya Ziwa 2012, yatakayoshirikisha mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Mara, pamoja na Visiwa vya Ukerewe.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Balimi, Edith Bebwa, alisema kuwa, maandalizi ya mashindano hayo yanayofanyika kwa mwaka wa saba sasa, yanaendelea vema kujiandaa na hatua ya ngazi ya mkoa.

Bebwa alisema kuwa hatua ya ngazi ya mkoa mwaka huu itaanza hapo Oktoba 20 mkoani Kigoma, ikifuatiwa na Kagera Oktoba 27, Mwanza zamu yao itakuwa ni Novemba 4, kisha yatakwenda Kisiwa cha Ukerewe hapo Novemba 10 na kumalizia Mara Novemba 17.

Washindi watatu kwa timu za wanaume na mbili kwa wanawake ngazi ya mikoa, watapata fursa ya kushiriki fainali kuu za mashindano hayo Mwaloni, Kirumba, Mwanza hapo Desemba 2, ambapo washindi watajinyakulia zawadi za pesa, vikombe na kuwekwa majina yao katika ‘Ukuta wa Mabingwa.’

“Zawadi za miaka iliyopita, zimefanya kusahaulika kwa baadhi ya washindi wetu, ikiwamo wenyewe kushindwa kubaki na ukumbusho muhimu. Balimi imeamua kuboresha zawadi za pesa, kutoa pia vikombe, lakini kuandikwa kwa majina yao kwenye Ukuta wa Mabingwa,” alifafanua Bebwa.

Bebwa alizitaja zawadi za washindi wa mikoa kuwa ni mshindi wa kwanza 900,000 kwa wanaume na 700,000 kwa wanawake. Mshindi wa pili wanaume atazoa 700,000, wakati kwa wanawake atashinda shilingi 600,000. Mshindi wa tatu wanaume ataibuka na 500,000, na wanawake ataweka kibindoni shilingi 400,000.

Aliongeza kwa kusema kuwa, mabingwa wa mwaka jana upande wa wanaume na wanawake watapata fursa ya moja kwa moja kushiriki fainali kuu jijini Mwanza, ambapo zawadi za mshindi wa kwanza wanaume itakuwa shilingi 2,700,000 kwa wanaume na shilingi 2,300,000 kwa wanawake.

Mshindi wa pili wanaume atajinyakulia 2,300,000, huku kwa wanawake akijishindia 1,700,000, ambapo wa tatu wanaume atatwaa shilingi 1,700,000, huku wanawake akinyakua shilingi 900,000. Mshindi wa nne wanaume atazoa shuilingi 900,000 na wanawake ataibuka na kitita cha shilingi 700,000.

Post a Comment

Previous Post Next Post