Mabingwa
wa soka Tanzania Bara Simba jioni ya leo watakuwa na kibarua pevu cha
kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo wa ligi kuu ya soka
Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa sugar ya Turiani Morogoro mchezo utakao
pigwa uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Huu
ni mchezo wa mwisho wa Simba katika ligi kuu ya soka Tanzania Bara
kabla ya kuelekea nchini Angola kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya FC
Libolo.
Simba
itakuwa inaingia uwanjani hii leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi
wa bao 1 - 0 iliyoupata jijini Mbeya mbele ya Tanzania Prison ushindi
ambao ulifakiwa kutuliza hali ya hewa kufuatia matokeo ya sare mbili
mfululizo toka JKT Oljoro na JKT Ruvu tangu kuanza kwa ligi mzunguko wa
pili wa ligi hiyo.
Kocha
mkuu wa wekundu hao mfaransa Patrick Liewig ambaye yuko katika
shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo la kutakiwa
kung'olewa kutokana na mashabiki kuanza kuhoji juu ya uwezo wake,
atalazimika kuendelea kumtumia Juma Nyoso katika sehemu ya ulinzi wa
kati akicheza pacha na Komabil Keita kufuatia mlinzi mahiri Shomari
Kapombe kutokuwa katika hali nzuri kimchezo baada ya kufanyiwa matibabu
ya kuondoa damu iliyovilia ndani ya mishipa.
Taarifa
iliyotolewa jana na msemaji wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga imesema kuwa
Kapombe hatakuwemo katika kikosi cha leo na kwamba huenda akarejea
uwanjani katika mchezo wa marudiano dhidi ya Libolo nchini Angola.
Simba
endapo itashinda katika mchezo leo itakuwa imefanikiwa kufikisha jumla
ya alama 34 na hivyo kuwa nyuma kwa tofauti ya alama 2 dhidi ya Azam fc
yenye alama 36 baada ya jana kutota mbele ya mabingwa soka Afrika
mashariki na kati Yanga kwa kufungwa bao 1-0 na hivyo kuifanya Yanga
kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na alama 39.
Kwa
upande wao Mtibwa Sugar ambao katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi
hiyo kule mkoani Morogoro katika dimba la Jamhuri walifanikiwa
kuwaonjesha joto ya jiwe Simba kwa kuwafunga mabao 2-0, na kuanza
kuchafua hali ya hewa ya Msimbazi, hii leo watakuwa wakitaka
kudhihirisha umwamba wao mbele ya Simba kwa kuwafunga mara mbili, jambo
ambalo litaufanya mchezo huo kuwa mgumu.
Post a Comment