KAMATI ya utendaji ya klabu
ya Simba inatarajiwa kutoa uamuzi mgumu kuhusiana na mwenendo mbaya ulionayo
timu hiyo katika ligi kuu ya Vodacom.
Aidha, Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage amekanusha
taarifa za kujiuzulu kwake kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye ligi
hiyo.
Rage ameiambia Sports Lady leo kwamba kamati ya utendaji ya Simba
itakutana leo hii kwa ajili ya kujadili mustakabali wa timu yao.
Amesema kikao hicho
kitajadili kwa kina hali iliyopo sasa ambayo imesabababisha timu yao kupoteza hata matumaini
ya kutetea ubingwa wao.
“Tutakuna baadaye leo na
kujadili hali hii maana tukiiacha hivi hivi inaweza kutuletea madhara makubwa sana…pia tutatoa maamuzi
mazito baada ya kikao chetu,”alisema.
Kuhusiana na taarifa za
kujiuzulu kwake, Rage alisema anashangazwa na taarifa hizo zinapotoka kwani kama atafikia uamuzi huo ataitisha mkutano na waandishi
wa habari na kuzungumzia hatua hiyo.
“Mimi sijasema nitajiuzulu
jamani hata hiyo taarifa yenyewe ukiisoma haileweki, hivyo nawaomba wanasimba
kutulia kuona kipi kitakachofuata,”aliongeza Rage
Simba imeonekana kusuasua sua
katika ligi hiyo baada ya kutokuwa na matokeo ya kuridhisha sambamba na
kuamulia vipigo katika mechi zake.
Hali hiyo ilianza kujitokeza
tangu mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ambao ulipelekea kutoka
kileleni hadi kushika nafasi ya tatu.
Aidha, tangu kuanza kwa mzunguko
wa pili wa ligi hiyo, Simba imeshinda mechi mbili dhidi ya African Lyon 3-1 na Tanzania
Prisons 1-0, huku ikitoka sare mbili dhidi ya JKT Ruvu na JKT Oljoro kwa bao
1-1 kabla ya kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar jana.
Source :- dinaismail.blogspot.com
إرسال تعليق