KENYA YAANZA VIZURI MASHINDANO YA DARTS AFRIKA MASHARIKI



Afisa Tawala wa Mkoa wa Arusha, Jackson Saitabahu, akizindua mashindano ya mchezo wa Darts kusaka Bingwa wa Safari Lager Afrika Mashariki na kati , jana katika ukumbi wa Appex, kijenge, jijini Arusha.
Mgeni Rasmi, Afisa Tawala wa Mkoa wa Arusha, Jackson Saitabahu(wa pili kushoto), Rais wa Shirikisho la Darts Afrika Mashariki, Gesasu Waigama (aliye katikati), katibu mkuu wa Darts Afrika Mashariki, Gerald Kimetu(wa pili kulia) na Katibu mkuu wa Darts Taifa, Kaale Mgonja katika uzinduzi wa Mashindano ya Darts Safari Lager Afrika Mashariki na kati yaliyoanza jana katika ukumbi wa Appex, Kijenge, jijini Arusha.

 ******      ******
MABINGWA watetezi wa kombe la Safari Lager Afrika mashariki na kati katika mchezo wa “Vishale” Darts, Kenya wameanza vema kampeni ya kutetea ubingwa wao kwa kuibuka wababe katika mchezo wa kwanza uliohusisha timu za Taifa (Interstate), kwa kuifunga Tanzania kabla ya kuwatandika vibonde Uganda.

Katika mchezo huo nafasi ya pili imeenda kwa kikosi cha Tanzania One, huku ndugu zao Tanzania Warriors wakijituliza katika nafasi ya tatu na kuwachapa Uganda kwa tofauti ya pointi Tatu.

Awali akizindua mashindano hayo ya siku tatu, Afisa Tawala wa Mkoa wa Arusha, Jackson Saitabahu amesema kuwa, Lengo la mashindano yawe ni kuboresha muungano wa jumuiya ya Afrika mashariki na kuongeza mshikamano wa kimichezo miongoni mwa nchi wananchama.

Kwa upande wake Raisi wa Shirikisho la mchezo wa Darts Taifa (TADA)  na Afrika mashariki,  Gesasu Waigama amesema kuwa kutoka na ushiriki wa mwaka huu TADA na Jumuiya nzima inatarajia kuona mchezo huo ambao kwa siku za hivi karibuni umekuwa ukipoteza umaarufu utarudia hali yake ya zamani.

Akizungumzia baadhi ya changamoto zinazokabili mchezo huo, Katibu mkuu wa Darts Taifa, Kaale Mgonja amesema kuwa mchezohuo umekosa hamasa kutokana na kuchezwa katika kumbi za starehe sehemu ambazo watu wengi sio rahisi kufika na kuitaka serikali kutoa mchango wake katika mchezo huo.

Mashindano ya Darts Afrika Mashariki 2013 yanadhaminiwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji cha Safari Lager ambapo zaidi ya wachezaji 200 wanashiriki kutoka katika nchi za Kenya, Uganda na mwenyeji Tanzania.

Katika mashindano kuna michezo ya wachezaji mmoja mmoja (singles and doubles), michezo ya kitimu (team games), pamoja na  ile ya jumuiya iliyopigwa katika siku ya ufunguzi

Post a Comment

Previous Post Next Post