Kwa mara nyingine staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu anatengeneza kichwa cha habari baada ya kuacha historia jijini Arusha kufuatia ulinzi mkali aliokuwa nao, Ijumaa lina data zote.
Habari za uhakika zilieleza kuwa Wema na timu ya wafanyakazi katika kampuni yake ya Endless Fame Production, alikodisha ndege ya kifahari kutoka Dar kwenda Arusha kwa ajili ya mapumziko tangu Aprili 18 hadi 20, mwaka huu.
Ilifahamika kuwa ndani ya ndege hiyo ambayo kuikodisha ni mkwanja mrefu, aliongozana na kampani yake tu.
CHANZO CHA YOTE NI DIAMOND
Ilibumburuka kuwa timu yake hiyo ilikuwa takriban watu watano ambao walimsindikiza kwenda kwenye mapumziko kutokana na ‘stresi’ alizokuwa nazo.
Ilielezwa kuwa stresi alizokuwa nazo zilitokana na ile ishu ya kudaiwa kurekodiwa akibembeleza penzi kwa aliyekuwa mwandani wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ usiku mkali huku jamaa akiwa amelala na mpenziwe wa sasa, Penniel Mungilwa ‘Penny’.
Baada ya kutokea kwa ishu hiyo ndipo Wema alipoamua kwenda kujichimbia Arusha kupoteza mawazo.
“Unajua ile ishu ilimchanganya sana bidada maana hakutegemea kama Diamond anaweza kufanya kitu kama kile so (kwa hiyo) alikwenda kutuliza akili na kweli sasa hivi walau yupo fresh (vizuri),” alisema sosi wa karibu wa Wema.
AINGIA ARUSHA KWA ULINZI MKALI
Walipoingia jijini Arusha, staa huyo wa Filamu ya The Super Star alipokelewa kwa ulinzi mkali hadi katika hoteli ya bei mbaya aliyokuwa ameweka oda kwa ajili yake na watu wake.
“Unaambiwa kuanzia Arusha Airport (uwanja wa ndege) hadi hotelini ilikuwa ni full ulinzi wa kufa mtu,” kilisema chanzo chetu,
APOKEA MWALIKO
Habari zilieleza kuwa akiwa hotelini hapo, habari zilienea kama moto wa kifuu kuwa yupo jijini Arusha hivyo akapokea mwaliko kutoka kwa mashabiki wake waliotaka japo kumuona tu kwenye Fashion Show iliyoandaliwa.
KASHESHE
‘Eventi’ ilifanyika kwenye Ukumbi wa Club D (World Garden) uliopo jijini humo na ndipo kasheshe lilipoibuka kwa watu kukanyagana wakitaka kumuona na kupiga naye picha.
“Aisee Wema wee acha tu! Kusema kweli watu wanampenda sana. Kuna wakati niliona kama ukumbi unakuwa mdogo na kwa taarifa yako ilikuwa haijatangazwa. Sijui kama ingekuwa imetangazwa kuwa Wema yupo A-town, ingekuwaje maana kila mtu alitaka japo amshike tu,” alisema sosi wetu huyo.
MENEJA
Kwa mujibu wa meneja wake, Martin Kadinda, ilibidi kuomba ulinzi maalum wa mabaunsa ambao walihakikisha hadhuriki.
“Tuliwaambia tupo na mtu mkubwa sana hivyo tukapatiwa ulinzi maalum wa kuhakikisha Wema hapati tatizo la mtu kumdhuru na ndicho tulichokifanya,” alisema Kadinda.
Ilifahamika kuwa kwa harakaharaka ulinzi wa Wema ulikuwa na takriban watu wasiopungua 10, yote ikiwa ni kuhakikisha usalama wake.
Post a Comment