Katibu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa,
amemkosoa Rais Jakaya Kikwete, kuhusu kauli ya kumshauri Rais wa Rwanda,
Paul Kagame, kuzungumza na waasi wa serikali yake.
Dk. Slaa
amesema haoni busara kwa Rais Kikwete kuwaambia viongozi wa Rwanda,
akiwamo Rais Kagame, kuzungumza na wafuasi wa chama cha FDRL walioko
Congo kwa vile wanatambulika kama wauaji.
Alisema hayo
wakati akizungumza katika kongamano la vijana wa Chadema (Bavicha) la
uchumi na ajira lililofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Alimshangaa
kuwataka kuzungumza na watu ambao Kagame anawaita wauaji wenye asili ya
kundi la jeshi la Nterahamwe, lililokuwa linaangamiza Watutsi.
“Rais
Kikwete hapa nyumbani hawezi kuzungumza na wapinzani , hajachukua hatua
dhidi wauaji wa mwandishi Daudi Mwangosi, alishauriwa amuwajibishe
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda , amempandisha
cheo,” alisema.
Alisema Rais alitakiwa kuwaambia waje awapatanishe lakini si kuwaambia wazungumze na watu anaowatuhumu kuua Watutsi.
Kumezuka
sitofahamu ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda, baada
ya Rais Kikwete kutoa ushauri huo wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika
(AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia hivi karibuni.
Ushauri huo
ulionekana kumchukiza Rais Kagame, anayedaiwa kuhutubia mikutano kadhaa
nchini kwake na kutumia lugha ya matusi, kejeli na dhihaka dhidi ya Rais
Kikwete na Tanzania.
AJITOSA UFISADI GLOBAL PARTNERSHIP DIALOGUE
Dk. Slaa
amejitosa katika sakata la tuhuma za ufisadi wa mabilioni ya fedha,
zilizopaswa kugharamia wageni wakiwamo marais walioshiriki mkutano wa
Global Partnership Dialogue jijini Dar es Salaam na kusema matumizi
mabaya ya fedha za umma yanakuza tatizo la ajira.
Alidai kuwa
fedha hizo zilizotumiwa kuwalipia malazi na usafiri wa ndege wageni hao
hazijatolewa maelezo licha ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuahidi
kulizungumzia.
Dk. Slaa alidai kuwa, matumizi ya fedha kwa mtindo huo wa kukosa uwazi hayafanyika popote ila Tanzania peke yake.
Kadhalika
alidai ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma yalihusisha
uidhinishaji wa Shilingi trilioni 1.7 zilizotolewa wakati wa mdodoro wa
uchumi kwa washirika kampuni zisizofahamika.
Dk. Slaa
alidai fedha hizo zilizotolewa siku tatu kabla ya kikao cha bajeti kwa
kuwazawadia washirika na kampuni ‘hewa’ zimehojiwa na Mkaguzi na
Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) lakini hakuna maelezo.
Alisema
fedha za kuokoa mashirika zilitolewa India, Marekani, Ghana na Uingereza
lakini kwa utararibu wa uwazi si kama ilivyotokea kwa Tanzania ambapo
zoezi lilitawaliwa na usiri mkubwa.
KONGAMANO LA BAVICHA
Aliwataka vijana kutumia ubunifu , kutochagua kazi na kujituma ili kukabiliana na ukosefu wa ajira .
Alishauri
serikali kuendeleza vipaji badala ya kugombana na wabunifu na kusumbuana
na wabunifu wanapojitokeza akitoa mfano wa kugombana na wagunduzi wa
bunduki za magobore.
Alieleza kuwa ukosefu wa ajira unachangiwa na ufisadi, kukosa vipaumbele na kutoa kazi kwa kujuana badala ya kuzingatia sifa.
Chadema blog
Post a Comment