Umoja wa Afrika umeyapokea vizuri matokeo ya mazungumzo kati ya Marais
wa Sudan na Sudan Kusini na makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili
hizo kwa ajili ya kutekeleza maafikiano ya mafuta kati ya Sudan mbili.
Bi. Nkosazana Dlamin Zuma, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika
amepongeza maamuzi na hatua zilizochukuliwa na Marais Omar al Bashir na
Salva Kiir wa Sudan na Sudan Kusini katika mazungumzo waliyofanya huko
Khartoum pamoja na matokeo ya kuridhisha ya mazungumzo hayo hasa uamuzi
uliochukuliwa na serikali ya Sudan wa kuakhirisha kutekeleza uamuzi wake
wa kuzuia usafirishaji mafuta ya Sudan Kusini kupitia mabomba ya nchini
kwake.
Suala la kuendeleza mazungumzo kati ya Juba na Khartoum ili kutatua
hitilafu zilizosalia kati ya pande mbili hizo khususan mivutano iliyopo
katika kadhia ya eneo la Abyei, ni moja ya masuala yaliyopokewa vizuri
na Umoja wa Afrika.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini Jumanne iliyopita alifanya safari nchini
Sudan lengo likiwa ni kufanya mazungumzo na mwenzake wa Sudan, Omar al
Bashir, ili kutatua hitilafu zilizopo kati ya nchi mbili hizo. Safari
hiyo ilijiri ikiwa zimesalia siku kadhaa tu hadi kumalizika muhula
uliokuwa umeainishwa na Sudan wa kufunga mabomba yake ya kusafirishia
mafuta ya Sudan Kusini.
Post a Comment