Hotuba ya Mwalimu Nyerere kwa waandishi wa habari mwaka 1995 hasa kuhusu mustakabali wa muungano
“Watu
wamezungumza Uzanzibari, baadhi ni viongozi wetu wanajivunia Uzanzibari.
Nadhani wengine wanafikiria hata kujitenga, sio wengi, lakini wapo.
Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi, kusiwe na nchi moja bali mbili. Hili ni jambo linazungumzwa.
Tunataka
viongozi, kiongozi wanaoelewa hilo. Kuzungumza Uzanzibari si jambo la
fahari. Hatima yake utavunja nchi. Mtu mwenye akili, Mzanzibari ana
akili hawezi akautuza Uzanzibari wa kujiita sisi Wazanzibari na wao
Watanganyika.
Na adhani ile ina usalama ndani yake. Kufanya hivyo, hatima yake Zanzibar itajitenga.
Zanzibar
ikijitenga, kutokana na ulevi tu…sisi Wazanzibari wao Watanganyika…sisi
si wamoja. Ulevi tu…ulevi hasa ulevi wa madaraka.
Ikitokea
hivyo, sisi Wazanzibari wao Watangayika. Wakumbuke kwamba muungano ndio
unaowafanya waseme sisi Wazanzibari wao Watanganyika.
Nje ya
muungano hawawezi kusema hivyo, nje ya muungano hakuna Wazanzibari. Nje
ya muungano kuna wao Wapemba sisi Waunguja. Nataka mjue hivyo… nataka
mjue hivyo.
Nje ya
muungano hakuna sisi Wazanzibari wao Watanganyika. Hakuna… hakuna.
Kinachowafanya sasa wajiite sisi ni ubaguzi wa kuwabagua Watanganyika.
Wakishakuwabagua
Watanganyika, ile dhambi ya ubaguzi haifi, inaendelea. Dhambi ya
ubaguzi ukishakuitenda inaendelea, ni sawa na kula nyama ya mtu, ukila
nyama ya mtu utaendelea tu. Mtamaliza, mtatengana na Watanganyika halafu
mara mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari…kuna Wapemba na kuna Waunguja.
Wapemba watapata msukosuko kidogo au aaah. Mtakuta kumbe kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama… hamtakaa salama.
Hamuwezi
kukaa salama baada ya kutenda dhambi ya kubagua watu wa nchi yenu ile
ile moja, mkawaita wale wao na hawa sisi. Dhambi ile haishii hapo, ndiyo
historia ilivyo, ni sheria ya historia sio sheria ya Mwalimu Nyerere.
Huwezi
kufanya ubaguzi wa namna hiyo halafu dhambi ile ikuache hapo hapo.
Hapana, itakuandama. Ninalolisema kwa Wazanzibari nalisema kwa
Watanganyika.
Zanzibar wanaweza kujitenga kwa ujinga, kwa ulevi na hasa ujinga wa viongozi wao na Watanganyika wakabaki wameduwaa.
Wazanzibari hawa wanafanyaje? Wanatuacha hawa wenzetu jamani wanakwenda zao wenzetu!
Watanganyika walioachwa wameduwaa kwa kitendo cha Wazanzibari kuwakimbia, watabaki wamoja, hawataparaganyika.
Narudia…Wazanzibari
wanaweza wakatoka, wakajitenga wenyewe tu…sasa wengine wana bendera
sisi hatuna kwanini, wengine wana wimbo wa taifa sisi hatuna wimbo wa
taifa kwanini?
Basi
wakajitenga, si wote wanaosema hivyo ni viongozi wanaosema… basi
wakajitenga, wakawaacha Watanagnyika wameduwaa…hivi wenzetu kweli
wanatuacha!
Wakiwaacha
Watanganyika walio katika hali hiyo, Watanganyika wanaowashanga
Wazanzibari katika kuwaacha, Watanganyika hawa watakuwa salama.
Watanganyika
wakiwakataa Wazanzibari kwa tendo la dhambi ile ile, sisi Watanganyika
wao Wazanzibari… wakautukuza usisi Tanganyika na kwa ajili hiyo
wakawafukuza Wazanzibari, hawabaki salama.
Hapatakuwa
na Tanganyika… wakishakujitenga tu Wazanzibari wale wako kando hivi…
mmewafukuza mnajidai wakubwa ninyi… hawa nani hawa… wao wana rais sisi
hatuna rais kwanini… watimue.
Mkawatimua,
mkapata rais wenu hapa akawatimua. Hambaki… hambaki. Kwani mtasemaje,
mtakuwa mmeishasema sababu ya kuwafanya wale wao na ninyi ni ninyi… wao
vipi?
Wazanzibari…
halafu mbaki ninyi? Maana wako watakaosema Wazanzibari tu… Wazanzibari
kana kwamba kuna kabila Wazanzibari, mmewabagua.
Mtaanza
nyumba za Wapemba, mtaziingilia pale sasa hivi. Viko vijumba vya Wapemba
humu baadhi yao walikimbia wakati uleeee, vijumba vya kwanza
vitapitiwa… Wapemba… Wapemba, mtamaliza vya Wapemba.
Halafu
mtakuta ninyi mliokuwa mnajiita sisi… sisi Watanganyika, mtakapoanza
kuchoma nyumba za Wapemba zile mtakuta aah si sisi… sisi hawa wote si
wamoja.
Mbona za
Wapemba tunachoma za Wachaga hatuchomi kwanini. Kwani Wachaga si wazawa
bwana, hapa kuna wazawa hapa, sasa mnachoma za Wachaga mnaacha?
Mtakuta hakuna watu wanaitwa Watanganyika, mtakuta mlijidanganya mnadhani kuna watu wanaitwa Watanganyika, hakuna.
Kuna Wagogo, kuna Wanyamwezi, kuna Wasukuma, kuna Wazanaki, kuna Wakurya, kuna Wamwera… wengi sana, siwezi kuwataja wote.
Mtakuta
hakuna kitu kizima hivi kinaitwa sisi Watanganyika… hata kidogo. Na
madhali mmefanya dhambi ya kusema wao Wazanzibari si wenzetu… dhambi ile
ile itawatafuna nyinyi.
Na mimi
nasema Mwenyezi Mungu anisamehe, mnastahili iwatafune. Hamuwezi kutenda
dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na dhambi nyingine zimo mle mle
ndani ya kitendo hazisubiri.”
Post a Comment