Kikosi
cha Uokoaji katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kimefanikiwa kumuokoa
mtalii Bi. Jeanne Traska (32) kutoka Ujerumani pamoja na muongoza wageni
Athuman Juma ambao jana walikwama katika kilele cha Mawenzi Mlimani
Kilimanjaro. Kikosi cha Uokoaji cha TANAPA kiliweza kufika eneo la
kilele cha Mawenzi na kwa kutumia mbinu za uokoaji za kisasa kabisa
kiliweza kuwanasua majira ya kumi na moja jioni.
Licha
ya hali mbaya ya hewa iliyotokana na mawingu mazito katika eneo hilo,
Kikosi cha Uokoaji cha TANAPA kiliweza kukabiliana na hali hiyo na
kuweza kuwanasua na kisha kuwapeleka katika kituo cha Horombo majira ya
saa mbili usiku ambapo walichukuliwa na gari kupitia njia maalum ya
uokoaji na kufika katika Lango Kuu la Marangu saa nne na nusu usiku.
Hali
ya hewa ilisababisha helikopta maalum iliyoletwa kwa ajili ya zoezi la
uokoaji kushindwa kufanya kazi kwa kuwa mawingu mazito hayakuwezesha
marubani kuliona eneo la kilele kwa urahisi.
Hivi
sasa mtalii huyo pamoja na muongoza wageni wake bado wapo chini ya
uangalizi wa hifadhi kwa kushirikiana na Kampuni ya Nordic Tours
iliyomleta mgeni huyo.
Aidha,
kwa kuwa ni tukio lisilo la kawaida, uongozi wa hifadhi unaendelea
kuchunguza sababu zilizowafanya kuchepuka njia na kuelekea kilele cha
Mawenzi badala ya Kibo. Kwa kawaida Kilele cha Mawenzi huwa hakitumiwi
na watalii isipokuwa kwa kujaza fomu maalum inayoonyesha kuwa mgeni
amekubali kwa hiyari yake kupanda kilele hicho.
Imetolewana Idara ya Mawasiliano
Hifadhiza Taifa Tanzania
23.03.2014
Post a Comment