Serikali imesema
inatambua Tasnia ya Filamu ikiendelezwa vizuri ni chanzo kikubwa cha ajira kwa
vijana na ni njia madhubuti ya kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa
leo na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Concilia Niyibitanga wakati wa mkutano na waandishi wa
habari uliofanyikia ukumbi wa Idara ya habari MAELEZO.
Concilia alisema
kuwa mwamko unaongezeka kwa wasanii na watengenezaji wa filamu kutoka ndani na
nje ya nchi.
Hii inajidhihirisha
kwa idadi ya vibali vya utengenezaji filamu imeongezeka kutoka 100 mwaka 2000
hadi 472 Januari 2014.
Aidha, kampuni zinazojishughulisha na
uendeshaji wa shughuli za filamu nchini zimeongezeka kutoka Kampuni moja ya
Filamu Tanzania (TFC) na kufikia 129 mwaka 2013.
Kwa upande wa
watengenezaji wa filamu za ndani, uwasilishaji wa ukaguzi umeongezeka kutoka
filamu 96 mwaka 2000 hadi kufikia 1059 Februari 2014.
Naye Katibu
Mtendaji wa Bodi ya filamu nchini Joyce Fisoo alitoa rai kwa wasanii wa filamu
kutumia lugha ya Kiswahili hasa katika uandaaji wa jina ili kulinda na kuikuza
lugha yetu ya Kiswahi.
Tasnia ya
Filamu nchini ilianza tangu mwaka 1920 wakati wa ukoloni, baada ya Uhuru,
Serikali ya Tanzania kupitia bunge iliamua kutunga sheria namba 4 ya mwaka 1976
ya Filamu na Michezo ya kuigiza ili kuweka usimamizi mzuri wa tasnia hiyo.
Source:Georgina Misama-MAELEZO
Post a Comment