Tukio hilo lililowaacha watu vinywa wazi, lilijiri Aprili 22, mwaka
huu shambani katika Kijiji cha Kigwa, Kata ya Ukondamoyo wilayani Uyui,
Mkoa wa Tabora.

JESHI la polisi mkoani Tabora linamshikilia mwanamke
aliyejulikana kwa jina la Pima Mabubu kwa tuhuma za kumchoma kisu mpaka
kumjeruhi vibaya mwanamke mwenzake, Amina Hussein akidai ana uhusiano wa
kimapenzi na mumewe, Adam Ndekeja...
KISU KILIVYOFANYA KAZI
Habari kutoka kwa baadhi
ya mashuhuda zinasema kuwa, Amina alichomwa kisu mara mbili, kwenye paja
mguu wa kushoto kisha kwenye mgongo ambapo kilizama na kutoka mpini tu!
KISA KINASIMULIWA
Kwa mujibu wa taarifa za
awali, siku ya tukio, Pima alitoka nyumbani kwake na kumfuatilia mumewe
huyo kwenye shamba la tumbaku la kaka wa Amina (jina halikupatikana)
ambako alisikia kuwa mwanamke huyo yupo na mumewe.
“Pima alisikia Amina ana uhusiano na mumewe. Siku hiyo akasikia wapo
shambani. Akatoka nyumbani na kufuatilia akijua atawanasa laivu,”
kilisema chanzo hicho.
MWANAMKE ALIYECHOMWA KISU
Akizungumza akiwa amelazwa akiuguza majeraha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, Amina alisema:
“Mimi sina uhusiano na huyo mwanaume jamani. Kwanza huyo mwanamke
simjui kabisa. Nimemwona kwa mara ya kwanza siku hiyo ya tukio.
“Siku hiyo mimi na mwanangu kichanga (wa miezi mitatu) tulikuwa
shambani, mimi nilikuwa nikimsaidia kaka yangu kuvuna tumbaku, akaja
Adam (mwenye mke) naye akawa anasaidia kuvuna. Kuna wakati nilikwenda
kupumzika mahali ili nimnyonyeshe mwanangu.
“Ilikuwa ni hatua chache tu tokea mahali ambako mume wake alikuwa
akivuna. Nilipiga kelele za kuomba msaada, mume wake akaja mbio kusaidia
kwa kumdhibiti mke wake asiendelee kunichoma kisu zaidi,” alisema
Amina.
Akaendelea: “Nilianguka chini na kuanza kugalagala huku damu nyingi
zikinitoka. Ndipo wasamaria wema nao walifika na kumkamata Pima,
wakamfunga kamba na kumpeleka ofisi ya kata ambako alipelekwa Kituo
Kikuu cha Polisi Tabora.”
BODABODA YAMKIMBIZA HOSPITALI
Habari zaidi
zinasema kuwa, Amina akiwa hoi na damu chapachapa, alipandishwa kwenye
bodaboda na kukimbizwa kweynye hospitali ya rufaa ya mkoa kwa ajili ya
matibabu huku hali yake ikionekana si ya kuridhisha.
KILA MTU NA WAKE
Taarifa zaidi zinasema kuwa,
wakati ndugu wa Amina wakihaha kumshughulikia majeruhi huyo kupata
matibabu kwa lengo la kuokoa uhai wake, baadhi ya ndugu wa Pima walipiga
kambi nje ya kituo cha polisi wakipigania kumdhamini ndugu yao huyo.
“Ukitaka kujua msemo kwamba kila mchuma janga hula na wa kwao
fuatilia mkasa huu. Wakati ndugu wa Amina wakihaha kuokoa maisha yake
hospitalini, ndugu wa Pima nao walikuwa wakihangaika kuhakikisha
mtuhumiwa huyo anapata dhamana ili arejee uraiani. Hakuna aliyekwenda
kumjulia hali Amina,” kilisema chanzo.
KUHUSU MUME WA MTUHUMIWA
Katika hali
isiyotarajiwa, mume wa mtuhumiwa huyo alikimbia kusikojulikana muda
mfupi baada ya mkasa huo kutokea jambo ambalo limezua maswali yasiyo na
majibu.
Wengi wamekuwa wakiuliza ni nini kimemkimbiza mwanaume huyo kama kweli yeye hana uhusiano wowote na mwanamke huyo?!
“Au kuna ukweli unafichwa? Kama hakuna ni kwa nini Adam alikimbia?
Hapa kuna haja ya jeshi la polisi kumsaka mwanaume huyo mpaka kumkamata
ili ukweli ujulikane,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo.
Credit: Risasi Jumamosi/ GPL
Post a Comment