Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo linaanza kikao chake cha Bajeti, ambapo
muda wa kuchangia na kuwasilisha bajeti za wizara mbalimbali, umepunguzwa.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John
Joel, alisema muda wa kuchangia Bajeti hiyo, umepunguzwa kutoka dakika 10 hadi
saba na muda wa uwasilishaji wa bajeti za wizara mbalimbali, pia umepunguzwa.
Alisema
kutokana na mabadiliko hayo, sasa kila wizara itapewa siku moja ya kuwasilisha
bajeti yake na kujadiliwa. “Tumepima muda tukaona unatosha,“ alisema.
Kwa
mujibu wa Joel, Bunge litaanza kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri
Mkuu leo jioni kuanzia saa kumi baada ya kumalizika kipindi cha maswali na
majibu na kikao cha kupeana ratiba.
Joel
alisema Bunge hilo pia limeongeza siku za kufanya kazi na litakaa mpaka
siku za Jumamosi, lengo likiwa ni kuokoa muda uliopotea.
“Vikao vitaanza saa tatu asubuhi hadi saa nane mchana na kutakuwa na mapumziko,
ambapo vitaanza tena saa 10 hadi saa mbili usiku na kwa siku za Ijumaa, vikao
vitaanza saa tatu hadi saa saba na Jumamosi vitaanza saa tatu mpaka saa saba,”
alisema.
Alisema
wabunge wawili wapya, Ridhiwani Kikwete wa Jimbo la Chalinze Mkoa wa Pwani na
Godfrey Mgimwa wa Jimbo la Kalenga Mkoa wa Iringa wataapishwa leo, kabla
ya kuanza kwa mkutano wa kawaida.
Huko
Kalenga, Mgimwa aliwashinda wagombea wenzake, Grace Tendega wa Chadema na
Richard Minja wa Chausta, kwa kupata kura 22,943 dhidi ya kura 5,800 za
Chadema huku Chausta ikiambulia 143.
Ridhiwani
alishinda uchaguzi wa Jimbo la Chalinze kwa kupata kura 20,812, akifuatiwa kwa
mbali na mgombea wa Chadema, Mathayo Torongey aliyepata kura 2,628, mgombea wa
CUF, Fabian Skauti aliyepata kura 473 na mgombea wa AFP, Munir Husein
aliyeambulia kura 78.
Uchaguzi mdogo wa Kalenga ulifanyika hivi
karibuni baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wake, Dk William Mgimwa na Uchaguzi
wa Chalinze, ulifanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Said
Bwanamdogo.
Post a Comment