Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema wanasiasa wanaojadili suala
la kuendelea au kutokuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK),
wanastahili kujiuzulu au kufukuzwa ndani ya vyama vyao.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Salmin Awadh Salmin kusema kuwa Wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza hilo ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa au vinginevyo.
Salmin aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja kwa kuwa wanaona kwamba lengo la
kuundwa kwake halina dalili njema kwa siku za usoni.
Jana, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF,
Salum Abdallah Bimani alisema: “Kimsingi mpango huo unakwenda kinyume na
uamuzi wa vyama vya CCM na CUF ambao ulipitishwa na kuridhiwa na vikao
vya juu vya vyama hivyo viongozi wanaopinga jambo hilo wanaonyesha
kupingana na uamuzi wa vyama vyao.”
Ajenda ya siri
Mkurugenzi huyo wa CUF alikana chama chake kuwa na ajenda ya siri ya
kuvunja Muungano au kuyasambaratisha Mapinduzi ya Zanzibar na kusema
kinachopiganiwa ni muungano wenye usawa, haki na heshima kila upande wa
washirika.
Kuhusu Ukawa kususia Bunge Maalumu la Katiba, Bimani alisema chama chake
kimetoa masharti matatu yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kubadilisha
msimamo wake. Alitaja masharti hayo kuwa ni kuijadili Rasimu ya Katiba
kama iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba; wajumbe wa CCM
kuacha matusi, vijembe na ubaguzi na hilo lithibitishwe kwa maandishi na
viongozi wake wa kitaifa.
Jambo la tatu ni kuhakikishiwa kuwa vikao vya Bunge vitumike kujadili
rasimu na si sera za vyama vya siasa kwa vile ndiyo mwanzo wa
kukaribisha malumbano na kusababisha Bunge kupoteza mwelekeo na kuweka
nyufa katika Umoja wa Kitaifa.
Mbatia alaani
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia amelaani kauli zilizotolewa na viongozi wa CCM katika mikutano yake ya Unguja na Pemba.
Mbatia alisema kuwa hoja ya CCM kutaka kufuta Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar inapaswa kulaaniwa kwani italeta machafuko. “Serikali
ya Umoja wa Kitaifa si ya CCM na CUF tu, ni ya wananchi wote, ni makosa
makubwa kudhani kuwa Serikali hiyo ni ya vyama hivyo viwili. Ilifanyika
hivyo ili kutokuendelea umwagaji damu,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema madai ya CCM kuwa Maalim Seif hatalipwa mafao yake hayana
msingi wowote kwa sababu anacholipwa ni haki yake. “Kwani hayo mafao ni
ya CCM au wanaolipa kodi ni CCM tu? Ukweli ni chanzo cha amani na haki
ni msingi wa amani, ukweli utatuweka huru.”
Aliitaka CCM kutokuwaingiza Watanzania katika machafuko kwa sababu tu ya
uroho wa madaraka, badala yake kijenge hoja za msingi katika
majadiliano ya Katiba badala ya kuwatisha watu kwa udini, jeshi na
kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Chanzo: mwananchi.co.tz
Post a Comment