Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Valentino Mlowola akiongea na
waandishi wa habari baada ya tukio hilo la mlipuko wa bomu katika kanisa
la KKKT jijini Mwanza.
====
Mhudumu wa nyumba ya kupumzikia wageni wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya
Mashariki ya Ziwa Victoria, jijijini hapa, amejeruhiwa vibaya baada ya
kulipukiwa na bomu lililokuwa limewekwa kwenye korido la nyumba hiyo.
Tukio hilo lilitokea juzi (Jumatatu),
kati ya saa 1:45 na saa 2:20 usiku, katika eneo la Makongoro wilayani
Ilemela wakati mhudumu huyo Bernadetha Alfred (25) alipofungua kifurushi
cha mzigo alichodhani kimesahaulika kwenye eneo hilo, kabla ya
kumlipukia.
Kwa mujibu wa Katibu wa Dayosisi hiyo, Mollel Rogart, kifurushi hicho
kilichokuwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni, kilikuwa juu ya kreti
(tupu) za soda, karibu na eneo la kulia chakula lililopo katika nyumba
hiyo.
“Ule mfuko ulikaa pale siku tatu ndiyo usiku huo mhudumu wetu
akakichukua kukiangalia akidhani ni mzigo wa mtu umesahaulika.” Alieleza
Katibu huyo na kudai kuwa kifurushi hicho kilimlipukia mara tu
alipokifungua na kujeruhi vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili.
“Bernadetha kajeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo miguuni na
usoni na siwezi kusema kwamba chanzo cha mlipuko huo ni mambo ya kidini
japo ulinzi wetu haukuwa mkali kiasi cha kudhibiti watu walioingia na
vitu.” Alisema.
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Valentino Mlowola akithibitisha
tukio hilo jana, alisema kwamba uchunguzi wa awali uliofanywa na kikosi
maalum kutoka Dar es salaam umebaini kuwa bomu hilo limetengenezwa
kienyeji.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili tubaini ni nani
kafanya ili kama ni mtu au kikundi kimehusika tuchukue hatua haraka.
Natoa wito kwa wananchi kutochukua vitu ambavyo hawa uhakika navyo,
wanapoona vitu vya aina hiyo, watoe taarifa kwetu.” Alisema Kamanda
Mulowola.
Mlowola alieleza kuwa, Bernadetha aliyejeruhiwa vibaya katika sehemu
mbalimbali za mwili, alikimbizwa katika Hospitali ya rufaa ya Bugando
ambako anaendelea na matibabu.
Kamanda huyo alieleza kwamba, mabomu (yakiwemo ya kienyeji) yako
katika mifumo mbalimbali hivyo wananchi hususan wahudumu wa sehemu za
mikusanyiko wawe na tahadhari na vitu vinavyoonekana kusahaulika na
wasisite kuwajulisha polisi vinapoonekana hivyo.
Mlipuko huo uliozusha hofu kwa waumini mbalimbali wakiwemo wa Kanisa
hilo, umetokea ikiwa ni wiki moja baada ya maadhimisho ya ‘Huduma ya
Mtoto’ kwa makanisa mbalimbali ya Kikristu jijini hapa yaliyofanyika
kwenye kanisa hilo, yakitanguliwa na maandamano kutoka uwanja wa
furahisha hadi KKKT.
Post a Comment