JWTZ LASHIRIKI ZOEZI USHIRIKIANO IMARA NCHINI BURUNDI

Brigedia Jenerali Joseph Chengelela (kushoto)akimkabidhi bendera ya Afrika Mashariki msaidizi wa zoezi mara baada ya kukabidhiwa kutoka kwa mgeni rasmi hayupo pichani siku ya ufunguzi wa zoezi USHIRIKIANO IMARA 2014-BURUNDI.
Meja Jenerali James Mwakibolwa wa nne kulia akiwa na Brigedia Jenerali Joseph Chengelela wa tano kulia na Mwambata wa JWTZ nchini Burundi kanali Venant Mutashobya wa tatu kulia mara baada ya ufunguzi wa zoezi USHIRIKIANO IMARA 2014-BURUNDI.

Picha ya Pamoja ya maofisa wa serikali ya Burundi na Maafisa Wakuu wa Majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya ufunguzi wa zoezi USHIRIKIANO IMARA 2014-BURUNDI
Zoezi Ushirikiano imara limefunguliwa jana nchini Burundi katika mkoa wa Mwaro, Mgeni rasmi katika ufunguzi huo alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi  Mhe. Prosper Bazombanza.

Katika ufunguzi huo Mhe Bazombanza amesema kuwa ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika mashariki umetokana na makubaliano ya wakuu wa nchi wanachama yaliyofanyika mwaka 2001,hivyo kuzitaka nchi shiriki kuenzi makubaliano hayo kwa kushiriki mara kwa mara katika mazoezi hayo. 

 Amesema ushiriki katika mazoezi haya unajenga kujiamini kwa majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwafanya wanajeshi wa Jumuiya hii kutambua kuwa wapo pamoja katika masuala ya ulinzi. Gwaride rasmi lilipita mbele ya mgeni rasmi kwa heshma huku Wakuu wa Majeshi na wawakilishi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakihudhuria sherehe hizo. 

 Kwa upande wa Tanzania sherehe hizo zimehudhuriwa na Mkuu wa mafunzo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali James Mwakibola pamoja na mwambata wa JWTZ nchini Burundi kanali Venant Mutashobya ambaye kabla ya ufunguzi wa zoezi hili wakati wote alikuwa akivipokea vikundi kutoka Tanzania akianzia kupokea kikundi cha JWTZ kilichokwenda Burundi kwa njia ya barabara katika mpaka wa kabanga na baadaye kupokea kikundi cha wanamaji wa JWTZ kupitia mpaka wa Kagunga. 

 Zoezi ushirikiano imara ni moja ya mazoezi muhimu yanayolifanya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania kuendelea kuwa moja ya majeshi yenye weledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yake kitaifa na kimataifa. Zoezi hilo linafanyika nchini Burundi kuanzia tarehe 13 hadi 26 Oct 2014 ambapo hushirikisha majeshi ya nchi za jumuiya ya afrika mashariki za Burundi,Kenya,Rwanda,Tanzania na Uganda. 

 Mazoezi ya pamoja kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yameendelea kufanya majeshi katika ukanda huu kuwa na weledi kiutendaji hii ni kutokana na majeshi haya kubadilishana uzoefu katika Nyanja za kiulinzi na usalama. Wakati huohuo Tanzania imeteuliwa kuongoza zoezi hilo huku Brigedia Jenerali Joseph Cosmas Chengelela kuchukuwa jukumu la kuongoza   kombaini ya vikundi vitakavyo shiriki zoezi hilo. 

Akiongea mara baada ya ufunguzi, Mkuu wa zoezi kutoka Tanzanina Brigedia Jenerali Joseph Chengelela amesema ushiriki wa JWTZ katika mazoezi haya unalifanya JWTZ kuwa miongoni mwa majeshi bora katika ukanda huu kwani ni njia moja wapo ya kuwafanya maafisa na askari kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa majeshi mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Post a Comment

Previous Post Next Post