MOROGORO:- MOCHWARI YA HOSPITALI YA MKOA MAJANGA

Mheshimiwa Abdul-Aziz Mohamed Abood.
Stori: Dustan Shekidele
Morogoro ni miongoni mwa mikoa inayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkoa huo umegawanywa katika majimbo kumi ya uchaguzi na Morogoro Mjini, ni miongoni mwa majimbo hayo, likiongozwa na Mheshimiwa Abdul-Aziz Mohamed Abood kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wiki iliyopita, Gazeti la Uwazi lilichanja mbuga mpaka kwenye jimbo hilo na kuzungumza na wananchi wa kata za Bigwa, Boma, Kichangani, Kihonda, Kilakala,    Kingo, Mazimbu, Mbuyuni, Sabasaba na nyingine kibao na kufanikiwa kuzungumza na wananchi mbalimbali ambao walieleza kero mbalimbali zinazowasumbua.
MATATIZO YA WANANCHI
Tatizo kubwa lililoelezwa na wananchi wengi wa jimbo hilo, ni kuharibika kwa majokofu ya kuhifadhia maiti katika mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Morogoro ambapo mwandishi wetu alifika hospitalini hapo na kubaini kwamba ni majokofu mawili tu yaliyokuwa yakifanya kazi.
“Kama ulivyoona mwenyewe, mochwari kuna tatizo. Yaani kwa mfano kukitokea ajali za mabasi zinazoua watu wengi, maiti nyingi hulazwa sakafuni, tunaiomba serikali itusaidie jamani,” Vicent Lihokolelo, mkazi wa jimboni humo aliliambia Uwazi.
Matatizo mengine yaliyobainishwa na wananchi wa jimbo hilo, ni pamoja na ukosefu wa madawati, upungufu walimu na maabara kwenye shule za sekondari na za msingi, ukosefu wa dawa za kutosha kwenye zahanati, vituo vya afya, uhaba wa maji kwenye maeneo machache, vitendo vya ukabaji na biashara ya uchangudoa ulioshamiri kwenye maeneo ya Msamvu.
Kupandishwa kwa ushuru kwa wafanyabiashara wanaomiliki fremu mjini hapo, ni miongoni mwa matatizo mengine yaliyoainishwa na wananchi ingawa pia idadi kubwa ya wananchi, walionekana kukifurahia kitendo cha mbunge huyo kutoa mabasi yake (Abood) kwa mwananchi yeyote wa jimbo hilo anapopatwa na msiba.
MAELEZO YA MBUNGE
Jitihada za kumpata mbunge huyo, hazikuwa nyepesi kwani mara kadhaa, waandishi wetu walipishana naye kutokana na wingi wa shughuli alizokuwa nazo kwa wakati huo, zikiwemo ziara za viongozi wa juu wa nchi.
Hata hivyo, Uwazi lilipata nafasi kiduchu ya kuzungumza naye ambapo alikuwa na maelezo yafuatayo:
“Kuhusu tatizo la kuharibika kwa majokofu, ni kweli kuna tatizo pale hospitalini na nimekuwa nikihangaika mara kwa mara kulitatua tatizo hilo. Hata nikimaliza kuzungumza na wewe, nakwenda kuonana na mganga mkuu pamoja na viongozi wengine wa serikali kwani hali ni mbaya hasa kunapotokea ajali. Nawaahidi kwamba nitasimamia tatizo hili lipate ufumbuzi haraka.
“Upungufu wa madawati, walimu hasa wa masomo ya sayansi na maabara, ni tatizo la nchi nzima lakini najitahidi kuhakikisha kuwa nalimaliza kabisa jimboni mwangu. Tupo kwenye utekelezaji wa agizo la rais la kuhakikisha kila shule ya sekondari ya kata inakuwa na maabara.
“Kuhusu suala la uhaba wa maji, awali maeneo yaliyokuwa yanasumbua ni Nanenane, Chamwino na Mkundi lakini kote tayari visima vimechimbwa na hakuna tena tatizo hilo.
“Miundombinu ipo vizuri, barabara zote za jimbo langu zipo kwenye kiwango cha lami na ambazo zilikuwa bado, kwa mfano ya Mlapakolo, Posta kuingia Uwanja wa Jamhuri na ile inayoenda Kilakala zote zinajengwa kwa kiwango cha lami. Usiku taa zinawaka kwenye barabara zote kwani tumeshirikiana vyema na wenzetu wa Tigo kulikamilisha hili.
“Kuhusu vitendo vya uhalifu, ni kweli maeneo ya Manzese, Chamwino na Msamvu kuna hilo tatizo lakini kwa kushirikiana na jeshi la polisi pamoja na wananchi (ulinzi shirikishi), tunaendelea kupambana na tatizo hilo, sambamba na wanawake wanaojiuza usiku.
“Kimsingi tangu niingie madarakani, najitahidi sana kuwatumikia wananchi wa Morogoro na naamini wao pia ni mashahidi wa jinsi ninavyojitoa. Wakati mwingine natoa fedha mfukoni ili kununua madawa kwenye zahanati na vituo vya afya,” alihitimisha Abood huku akisisitiza kuwa suala la majokofu kwenye mochwari ya Hospitali ya Mkoa wa Morogoro lazima alipatie ufumbuzi mapema. 

Post a Comment

Previous Post Next Post