Zitto kung’oka CHADEMA

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), inadaiwa yupo katika hatua za mwisho kujiengua ndani ya chama hicho alichojijengea sifa kubwa

Kwa mujibu wa watu walio karibu na Zitto, wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa mbunge huyo alipanga kujiondoa ndani ya chama hicho mwezi uliopita lakini alishindwa kufanya hivyo kwasababu ambazo hazijawekwa wazi.

Inadaiwa Zitto, alipanga kuondoka CHADEMA sambamba na uzinduzi wa kitaifa wa chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) uliopangwa ufanyike mwezi uliopita.

Novemba 22, mwaka jana, Kamati Kuu ya CHADEMA iliamua kumvua nyadhifa za uongozi Zitto na wenzake wawili (Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba) kwa madai ya kukisaliti na kukihujumu chama.

Zitto alidaiwa kuwa kinara wa mkakati wa kuleta mabadiliko haramu ndani ya chama hicho, huku waasisi hao wakijipa majina ya MM, M1 na M2 ambao ndani yake anadaiwa kuwamo Dk. Kitila Mkumbo, mjumbe wa CC na NEC.

Hata hivyo Mkumbo na Mwigamba walivuliwa uanachama huku Zitto akikimbilia Mahakama Kuu kutaka CC isijadili unachama wake.

Katika hoja ya msingi iliyowasilishwa na Zitto kupitia wakili wake Albert Msando, aliiomba Mahakama Kuu kuwazuia washitakiwa kwa pamoja ambao ni Kamati Kuu ya CHADEMA au chombo chochote kwa makusudi, kujadili au kuamua suala la uanachama wake.


Maombi mengine ya Zitto ni kutaka apatiwe nakala za uamuzi wa Kamati Kuu iliyoamua kumvua uanachama ili aweze kukata rufaa kwa Baraza la Uongozi la CHADEMA.

Katika ombi la tatu, Zitto anaiomba mahakama iwazuie washitakiwa kuingilia kati wajibu na majukumu yake ikiwemo majukumu yake kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Mahakama Kuu ilikubali kwa muda kusitisha uamuzi wa CC ya CHADEMA kujadili uanachama wa Zitto mpaka itakapotoa uamuzi wa katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na mbunge huyo.

Katika amri hiyo, Jaji John Utamwa alisema kwa kuzingatia masilahi ya pande zote mbili ni vema walalamikiwa wakasitisha uamuzi wowote wa kujadili uanachama wa Zitto mpaka shauri hilo litakapotolewa uamuzi na mahakama.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa Zitto, anatarajia kwenda ACT-Tanzania kushikilia wadhifa wa Mwenyekiti wa chama hicho ambacho makada wenzake Mkumbo na Mwigamba wamekimbilia.

Harakati hizo za Zitto, zinadaiwa kushamiri zaidi hivi sasa baada ya CHADEMA kumaliza uchaguzi wake wa kitaifa na nafasi aliyokuwa akiishikilia imejazwa na John Mnyika

Kumalizika kwa uchaguzi wa CHADEMA, uliofanyika kwa utulivu hivi karibuni kunatajwa sababu ya Zitto kukata tamaa ya kurejea madarakani hivyo anaona njia pekee ya kujinusuru kisiasa ni kuhama CHADEMA.

Mbunge huyo kabla ya kukimbilia mahakamani alitaka kiitishwe kikao cha Baraza la Uongozi ili apewe fursa ya kujitetea ambako aliamini atapata uungwaji mkono

Hata hivyo tangu Zitto atoe ombi hilo Baraza hilo limeketi mara mbili bila kuwepo ajenda inayomuhusu kujadiliwa jambo lililoashiria hakukuwa na uungwaji mkono

Zitto afunguka

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, juu ya taarifa za kujitoa CHADEMA, Zitto alisema kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa potofu dhidi yake.

Alisema baadhi ya taarifa zina lengo la kumchonganisha na kumharibia sifa yake mbele ya jamii na makada wenzake.

Zitto alisema jambo lolote linalomhusu hatosita kulizungumzia mwenyewe kama alivyowahi kufanya katika masuala mbalimbali.

Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na mambo yanayovumishwa dhidi yake ambayo hayana ukweli

Zitto, alibainisha kuwa ikiwa ataondoka au ataendelea kubaki CHADEMA jambo hilo analijua mwenyewe.

“Watu wasema mambo kwa kuhisia hisia, mimi ndiye ninajua ninachokifanya……Hizo nyingine ni hisia za watu siwezi kuzizuia” alisema

“Nawaomba watu wajiepushe na maneno maneno ya mitaani, nina uwezo mkubwa wa kuzungumzia masuala yanayonihusu” alisema.

Dk. Slaa anena

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa, amesema ni haki ya kikatiba na ruhusa kwa mwanachadema yoyote kuhamia chama chochote cha siasa anachoona kinamfaa.

Dk. Slaa, alisema fununu za aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zitto Kabwe, kutaka kujiunga na chama kipya cha ACT Tanzania, anazisikia na hawezi kumzuia kuhamia huko.

Alisema haoni kama anayo sababu yoyote ya kumjadili Zitto katika uamuzi wake wa kutoka CHADEMA na kuhamia chama kingine.

“S mimi Dk. Slaa wala CHADEMA, wanayo sababu yoyote ya kumjadili mtu na uamuzi wake mwenyewe …anayo haki ya kuhamia chama chochote ambacho ataona ana manufaa nacho, hana haja ya kupata kibali cha mtu”

“Zitto hatokuwa mwana- CHADEMA wa kwanza kuhama cha hiki na wala hatakuwa wa mwisho ….wengi watahama na wengi watahamia hivyo sioni kama kuna dhambi yoyote hapo” alisema

Katibu Mkuu huyo alisema kwa sasa hayuko tayari kuzungumzia mwanachama anayehama na kuhamia, bali yuko tayari kujadili maslahi ya Watanzania na nchi hasa suala la katiba iliyopendekezwa.

“Kichwa changu sasa kinafikiria ni namna gani kitawasaidia Watanzania waikatae katiba inayopendekezwa ambayo imechakachukuliwa kwa ajili ya manufaa ya watu wachache”alisema.

Chanzo: freemedia.co.tz

Post a Comment

Previous Post Next Post