Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala
Rai hiyo waliitoa kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na NIPASHE kutokana na adha ya kuungua kwa jua na kunyeshewa na mvua wanayoipata kwa muda mrefu.
Walisema wamekuwa wakipata adha kubwa katika eneo hilo lwakati wakisubiri kuvushwa na kivuko Mto Kilombero kutoka upande mmoja kwenda mwingine kutokana na kutokuwapo kwa vibanda hivyo.
Shukuru Mkamati, Mkazi wa kijiji cha Kivukoni, alisema kwa miaka kadhaa eneo hilo la kivuko halina sehemu ya kupunzikia, hivyo kulazimika wananchi na viongozi kuunguzwa na jua au kunyeshewa mvua wakati wakisubiri kuvushwa na kivuko hicho.
Neema Lipangalala, alisema nia aibu kwa eneo hilo kukosa sehemu ya kupumzikia hata kwa viongozi wa kitaifa wanaotembelea shughuli mbalimbali.
“ Tumesema sana watujengee vibanda vya kupumzikia lakini wapi, tunashindwa kuelewa kama hawana uwezo si waruhusu wawekezaji wajenge hata hoteli katika eneo hilo ili pawepo na mabanda ya kusubiria kuvuka, ” alisema Lipangalala.
Kwa upande wao, wajumbe wa bodi ya kivuko cha mto Kilombero katika kikao chao, waliagiza Tamesa kuharakisha ujenzi wa vibanda vya kujikinga mvua katika eneo hilo.
Mbunge wa Ulanga Magharibi (CCM), Dk. Haji Mponda, alisema inashangaza ujenzi huo kushindwa kufanyika wakati kiasi kikubwa cha fedha kinakusanywa kutoka abiria, mizigo na magari.
Alisema ni mwaka mmoja umepita toka walipotoa agizo la kujengwa vibanda vya kujikinga na mvua na jua kwa abiria wanaotumia kivuko hicho, lakini hakuna kilichofanyika kwa madai kuwa wenye maamuzi ya kutoa fedha ni Temesa makao makuu.
Wazo hilo liliungwa mkono na mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala, akisema inaonyesha mawazo ya bodi hayatekelezeki hivyo hakuna sababu ya kuendelea kutoa ushauri.
Masala alisema ushauri wa wajumbe ni muhimu kutekelezwa kwani wao ndiyo wanaishi maeneo husika na kuona adha wanayopata abiria hivyo kuna umuhimu wa kujengwa kwa vibanda hivyo vya gharama nafuu.
Awali akisoma taarifa ya hali ya utendaji wa kazi wa kivuko hicho kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba 2014, Meneja wa Temesa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Magreth Mapula, alisema tokea Januari hadi Juni wamekusanya kiasi cha Sh. 347,151,286 na Julai hadi Novemba Sh. 429,078,050.
Meneja huyo alizitaja changamoto zilizojitokeza kwa kipindi hicho kuwa ni mvua kubwa kunyesha zilizosababisha mafuriko na hatimaye kufunga huduma za uvushaji kwa muda na utobokaji wa mara kwa mara wa tangi za kivuko unaosababishwa kujisugua kwenye maegesho.
Changamoto nyingine ni ajali za magari kugonga kivuko na kutumbukia majini kutokana na ubovu wa mfumo wa breki, majani na nyavu kusonga mfumo wa usukani wa kivuko na mchanga kujaa mtoni hasa wakati wa kiangazi maji yakipungua.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment