CCK yamvaa Prof. Tibaijuka

Prof. Tibaijuka.
Chama cha Kijamii (CCK), kimemshukia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka , kwamba asijione ni muhimu sana katika wizara hiyo kiasi kwamba hata akiondoka nafasi yake haitazibwa na mtu mwingine.
Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Kauli ya chama hicho imefuatia tamko la hivi karibuni lililotolewa na Profesa Tibaijuka kwamba yeye na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ni majembe ya Rais Jakaya Kikwete na hivyo hawawezi kujiuzulu.

Muabhi alisema ProfesaTibaijuka ni lazima afahamu kwamba shinikizo la wananchi kutaka awajibike katika kashfa hiyo ni yeye (Tibaijuka) kukosa uadilifu kwa kupewa zaidi ya Sh. bilioni 1.6 kama msaada katika shule yake bila kuzitolea maelezo kama sheria zinavyotaka.

“Profesa Tibaijuka asifikiri ni mtu ‘special’ katika wizara hiyo kiasi kwamba akiondoka hakuna mtu mwingine atakayeziba nafasi yake, kinachozungumzwa ni suala la uadilifu kwa sababu kiongozi wa umma unapopewa zaidi ya Sh. 50,000 unapaswa kuzitolea maelezo lakini yeye kapewa Sh. bilioni 1.6 na hakuzitolea maelezo,” alisema.

Aidha, Muabhi alimuomba Rais Kikwete wakati anatoa uamuzi wake kuhusu sakata la Akaunti ya Escrow atumie hekima na busara badala ya shinikizo la wanasiasa ili atende haki.

Alisema Rais Kikwete anatakiwa atumie busara katika kutoa uamuzi wake ili wasije kuadabishwa watu wasiostahili, kwa sababu kuna baadhi ya wahusika hawakuhojiwa katika sakata hilo.

Alisema katika sakata hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Beno Ndullu, wanapaswa kuhojiwa kwa sababu ofisi zao zilihusika na kufanikisha kutolewa kwa fedha hizo.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post