Kwa vile ustawi wa biashara hutegemea uhakika wa
soko/masoko, ni muhimu kuzingatia masuala ya masoko katika ufanyaji wa
biashara. Mjasiriamali anatakiwa kuwa na taarifa anuai juu ya soko la
bidhaa/huduma anazozitoa.
Mjasiriamali anatakiwa kujua tabia za wateja wake.
Wateja huwa wana tabia tofauti katika vipindi tofauti. Kujua tabia za
wateja kutamsaidia mjasiriamali kupanga mipango yake yenye kutekelezeka
kiurahisi. Pia, itamsaidia kutoa taarifa sahihi juu ya mchakato mzima wa
masoko ya huduma/bidhaa zake.
Mjasiriamali anatakiwa kujua ushindani uliopo
katika biashara anayoifanya. Ni nadra sana katika ulimwengu wa leo
kukuta mjasiriamali anafanya biashara ambayo haina mshindani kabisa. Kwa
maneno mengine, hata kama biashara yako ni ya kipekee lazima kutakuwa
na mbadala wake.
Kutokana na hali hii, ni vizuri mjasiriamali akawajua washindani wake ili kuweza kukabiliana nao kwa mafanikio zaidi.
Mjasiriamali anatakiwa kujua jinsi alivyojipanga
katika ulimwengu wa biashara. Hii ina maana kuwa mjasiriamali anatakiwa
kujua jinsi atavyoingia sokoni kwa kuzingatia ubora alionao katika
utoaji hudu. Vilevile anatakiwa kujua namna atakavyokabiliana na udhaifu
alionao katika masoko, kwani hakuna biashara isiyokuwa na udhaifu hata
kama ni mdogo kiasi gani.
Mjasiriamali anatakiwa ajue mbinu za kutafuta
masoko. Mjasiriamali sharti awe na rasilimali watu yenye uwezo mkubwa wa
kutafuta masoko. Kama nilivyosema hapo awali biashara ni masoko na
masoko ndiyo wateja. Pasipo masoko hakuna biashara.
Kwa maana hiyo mjasiriamali anatakiwa kuwa mjanja
wa kupenyeza kwenye masoko ambayo hakuwa nayo hapo awali. Hii itahitaji
mbinu mbalimbali ili kuweza kuwashawishi wateja wakubaliane na kile
unachokifanya.
Mjasiriamali anatakiwa kujua makadirio ya mauzo ya
bidhaa zake. Kwa maneno mengine, mjasiriamali anatakaiwa kujua
makadirio ya idadi ya wateja wake anaowahudumia katika vipindi tofauti.
Idadi ya wateja hutegemea dira au dhima ya
biashara husika. Kwa mfano, mjasiriamali anaweza kuelekeza nguvu zake
katika kuwahudumia watu fulani tu kama vile wanafunzi wa shule za
msingi. Pia, anaweza kutengeneza bidhaa/kutoa huduma kwa ajili ya watu
wote.
Mjasiriamali anatakiwa kujua ukubwa wa soko la
huduma/bidhaa zake. Hili linafanyika kwa kuangalia wateja wa eneo
(biashara) husika au kuangalia mauzo yaliyofanyika mwaka ulipita na
jinsi soko linavyokua. Kwa maneno mengine, mjasiriamali anatakiwa
kuangalia idadi ya wateja wake ili aweze kuzalisha bidhaa au kutoa
huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja wake.
Vilevile mjasiriamali anatakiwa kuelezea
rasilimali alizonazo katika kukidhi mahitaji ya soko, namna ya kuingia
sokoni na namna ya kupanua soko la bidhaa zake. Pia, anatakiwa kuelezea
namna biashara itakavyoonekana siku za usoni, thamani ya bidhaa na namna
biashara inavyoweza kukabiliana na upinzani sokoni.
Post a Comment