Doha, Qatar. Serikali ya Qatar inajenga bandari
mpya katika eneo la jangwa, mradi unaogharimu Dola za Marekani 80
bilioni na ikimteua raia wa Tanzania asimamie kazi hiyo.
Ujenzi huo unatokana na Serikali ya nchi hiyo kuamua kuhamisha bahari na kuipeleka katika eneo hilo la jangwa.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyemaliza ziara ya
kuzitembelea nchi za Falme za Kiarabu juzi usiku, alitembelea mradi huo
wa bandari mpya ambao unajengwa eneo la jangwa na baadaye kuelekeza maji
ya bahari kufika eneo hilo.
Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa mradi huo,
Potty Msuku alisema kazi kubwa anayofanya ni kusimamia na kuhakikisha
kazi inakwenda kwa wakati.
Alisema bandari hiyo itakayoanza kufanya kazi kuanzia mwakani, ina magati zaidi ya 10 ya kuegeshea meli.
“Ninachoshukuru ni kwamba tuko mbele ya muda tuliopewa, tunakwenda vizuri.”
Mtanzania huyo alisema mpango wa ujenzi wa bandari
hiyo mpya ulibuniwa na Serikali ya Qatar ili kufungua lango la biashara
kwa mataifa makubwa.
Alisema mradi huo ukikamilika utaifanya Qatar kuwa
moja ya mataifa yenye bandari kubwa dunia sanjari na mataifa ya
Kiarabu, Dubai na Abu Dhabi.
“Tumechimba eneo hili ambalo hadi Aprili mwakani tutakuwa tumepasua mwamba wa bahari na maji yatakuja huku,” alisema.
Alisema ujenzi huo ulioanza 2011 utakamilika 2016.
Msuku ambaye ni mhandisi kitaaluma, alisema ujenzi
wa bandari hiyo unakwenda kwa awamu, nyingine inayofuata ni ya
kuiunganisha bandari hiyo na reli na uwanja wa ndege utakaojengwa karibu
na eneo.
“Kazi kubwa inayoendelea sasa ni ya kuchimba kina,
tumefikia pazuri na nyingine ni kujenga eneo la biashara huru na
kitengo cha makontena.”
Post a Comment