Dar es Salaam. Serikali imekiri kuwapo kwa
upungufu katika uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia mfumo wa
Teknolojia ya (BVR) wakati wa majaribio na kuitaka Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) inayoratibu zoezi hilo kulirudia maeneo yote litakapoanza
rasmi mapema mwakani.
Kauli hiyo ya Serikali inakuja siku moja kabla ya
zoezi hilo kumalizika katika Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam,
Kilombero mkoani Morogoro na Katavi linalotarajiwa kukamilika keshokutwa
huku likikumbwa na matatizo ya mashine kushindwa kuhimili mazingira ya
joto na changamoto mbalimbali.
Akiwa katika ziara ya kukagua zoezi hilo jana
katika kituo cha Bunju A jijini humo, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na
Bunge, William Lukuvi alibainisha mambo makuu manne yanayotakiwa
kufanyiwa kazi haraka ili kulifanya zoezi hilo kuwa na uhalali. Alitaja
mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa dawati maalumu la kuhakiki
taarifa zinazotolewa na mhusika, ili kuepuka kuwaandikisha watu wasio na
sifa.
“Kinachofanyika sasa mtu anapofika kujiandikisha,
anaulizwa jina, umri na maswali kadhaa,” alisema Lukuvi akifafanua kuwa
hata mtu akidanganya hakuna sehemu yoyote ya kubaini uogo huo. “Mtu hata
akiwa siyo Mtanzania, hivi mnavyofanya anaweza kujiandikisha…, akiwa
mtoto anaweza kujiandikisha hii ni hatari,” alisema akionya.
Aliongeza: “Pili, waandikishaji lazima wawe wengi
kwani kama foleni ndiyo hii, hili ni tatizo, mtu anatakiwa kuja hapa
mara moja anapata huduma na kuondoka, lakini pia muwe na ukakika wa
mashine. Mnahitaji ngapi na katika maeneo yote mtatumia muda gani.”
Lukuvi aliitaka NEC kuwa makini na zoezi hilo
akisema kwamba Serikali imewaamini na wakikosea makosa yote yatarudi
serikalini na hasa kwa CCM jambo alilosema hawataki litokee.
“Mmesema ni zoezi la majaribio, lazima mtumie
changamoto hizi kuboresha uandikishaji la sivyo tutakuja kupata lawama
baadaye,” alisema Lukuvi.
Awali akisoma taarifa fupi ya zoezi hilo,
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba alisema katika majimbo hayo
uandikishaji unaendelea vizuri na utakamilika kama ilivyopangwa.
Alisema Kawe uandikishaji ulianza Desemba 16 mwaka
huu na utamalizika kesho, Kilombero Desemba 15 mwaka huu na unamalizika
leo huku Milele mkoani Katavi Desemba 17 mwaka huu na utamalizika
keshokutwa.
“Kuna changamoto mbalimbali zimejitokeza lakini
zoezi linakwenda vizuri kama tulivyopanga na tunatarajia litakapoanza
rasmi Januari mwakani au Februari mwanzo mwakani tutaweza kumaliza kwa
wakati.”
“Lakini mashine hizi zimekuwa zinapata joto hivyo
kushindwa kufanya kazi ambapo wataalamu wetu wamesema tutazingezea feni
ili kuhimili joto...Mwanzo mashine zilikuwa haziwezi kupiga picha watu
wenye macho mekundu lakini tumezifanyia marekebisho na tunaendelea
vizuri,” alisema Malaba
Post a Comment