Watanzania kunufaika na ajira

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Watanzania watanufaika na kipato na maarifa ya teknolojia ya kisasa kutokana na ajira ambazo watapata katika nchi ya Qatar baada ya mkataba kusainiwa hivi karibuni.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Doha, Qatar wakati akizumgumza na waandishi wa habari ili kuwapa taarifa fupi juu ya mambo yaliyojiri kwenye mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani.

Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika ofisini kwa Sheikh Abdulla, Pinda alisema wamekubaliana kutoa ajira kwa Watanzania kwa sababu nchi hiyo inahitaji wafanyakazi wengi kwenye sekta mbalimbali na raia wake ni wachache.

“Hapa Qatar kuna uwekezaji mkubwa umefanyika, kwa hiyo wanahitaji watu wa kufanya kazi... kwenye mahoteli, viwandani na kikubwa hapa ninachokiona watu wetu watapata kipato lakini pia watapata ujuzi kwa maana ya maarifa yanayoendana na teknolojia ya kisasa.”

Maeneo mengine aliyosema wamekubaliana kushirikiana ni kilimo, gesi na mafuta kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania na Tehama.

Alisema wamekubaliana na Sheikh Abdulla al Thani kuunda timu ya pamoja baina ya nchi zao ili ifanye kazi ya kuainisha ni maeneo gani wanataka waanze nayo kwanza kulingana na mahitaji.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post