Songea. Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel
Nchimbi amerudi kwa kuanza kuratibu sherehe za kutimiza miaka 38 ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) kitaifa mwaka huu.
Sherehe hizo zitakazofanyika mkoani Ruvuma, mgeni
rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya
Kikwete. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Umoja ni Ushindi, Katiba yetu
nchi yetu.’
Dk Nchimbi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya sherehe hizo, alisema kila kitu kimekamilika.
Alisema Ruvuma mwaka huu imepata heshima kubwa ya
kuandaa sherehe hizo itakayofanyika Februari Mosi, mwaka huu badala ya
Februari tano kama ilivyozoeleka.
Dk Nchimbi ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu
tangu alipoondolewa kwenye uwaziri, alisema mabadiliko hayo yanalenga
kuwapa fursa wananchi wengi ili waweze kushiriki.
“Februari tarehe tano ni siku ya kazi, sasa tusiharibu utaratibu wa watu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza kuwa:
“Maandalizi ya vijana wa halaiki, uwanja na
vikundi mbalimbali vya ngoma yanaendelea, vijana wa bendi kutoka
Zanzibar wameshawasili na wanaendelea na mazoezi, bendi yetu ya Tanzania
One Theatre (TOT) nayo itatumbuiza.
“Pia, watakuwapo wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wakiongozwa na Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platinum.”
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho
alisema chama hicho kimeendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo
kama ilani inavyoelekeza kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
“Tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika sekta ya
elimu, afya, maji na miundombinu... Pia barabara nyingi zimejengwa kwa
kiwango cha lami ikilinganishwa na miaka iliyopita,” alisema Mwisho.
Post a Comment