Zoezi la upigwaji kura ya maoni dhidi ya Katiba
inayopendekezwa ambalo limepangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu sasa ni
dhahiri kwamba liko katika njia panda.
Suala hilo lipo njia panda kutokana na maelezo yaliyotolewa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bungeni jana, kwamba zoezi hilo linategemea
uwezo wa Tume wa kukamilisha uandikishaji wa wapigakura kwenye daftari
la kudumu.
Msimamo huo ulitolewa jana na Waziri Mkuu, Pinda wakati akijibu
maswali ya papo kwa papo bungeni, ikiwa ni baada ya kuulizwa swali na
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliyetaka
kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha zoezi la uandikishaji wa
wapiga kura kwenye daftari la Kudumu kwa mfumo wa Biometric Voters
Registration (BVR) linakamilika kwa kushirikisha wadau wote.
Mbowe alisema anazo taarifa kwamba Serikali imekuwa ikikosa fedha
za kuandikisha wapigakura kwa mfumo huo na kulazimika kuahirisha zoezi
hilo mara kwa mara na mpaka sasa zoezi hilo halijaanza huku ikiwa
imesalia miezi mitatu tu kuifikia siku iliyopangwa kwa ajili ya kupiga
kura ya maoni.
Mbowe alisema kuwa Serikali ilitangaza kwamba zoezi la kuanza
kuandikisha wapiga kura kwa utaratibu wa BVR ungeanza Februari, 2014,
lakini utaratibu huu haukuanza, ikatangaza tena kuwa itaanza Septemba,
2014, kazi hiyo haikuanza, Kisha tena Serikali ikasema itaanza Desemba,
2014, kazi hiyo haikuanza na hatimaye ikatangaza kuwa itaanza kazi hiyo
Januari 30 yaani leo na kazi hiyo haitaanza.
Alisema mara zote hizo Serikali ilikuwa ikiahirisha zoezi la kuanza
kuandikisha wapigakura kwa sababu ya ukosefu wa fedha na sasa Tume
imesema itaaza kuandikisha wapigakura nchi nzima tarehe 15 Februari
mwaka huu, ambapo pia ana shaka kwamba fedha zitakuwapo.
Mbowe alisema kuwa wakati taifa likiwa linaahilishwa kila siku
kuhusu lini utaratibu huu unaanza, Tume ya Uchaguzi iliomba kuletewa
kits kwa ajili ya uandikishaji 15,000 Serikali ikasema haina uwezo
katika hatua hiyo na baadaye ikasema itatoa kits 8000, ambazo pia
hazijafika nchini.
Alisema kuwa kilichojitokeza ni wakati wa majaribio zilitolewa kits
250 ambazo zilifanyiwa majaribio katika jimbo la Mlele mkoani Katavi,
Jimbo la Kilombero, Morogoro na Kawe jijini Dar es Salaam, majaribio
ambayo yalionyesha kuwa mitambo hiyo ina matatizo makubwa na kumekuwa na
malalamiko makubwa kutoka kwa wadau kwamba mfumo mzima wa Biometric
haujafahamika.
“Serikali imetangaza tarehe 30 Aprili kuwa siku ya kura ya maoni,
kura ambayo inategemea kutumia daftari hili, ambayo ni miezi mitatu
kamili kuanzia sasa hivi, alafu wakati huo huo Uchaguzi Mkuu ni miezi
minane kuanzia sasa hivi, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba
daftari hili linaandikishwa na wadau wanashirikishwa kikamilifu kwa
sababu utaratibu huu ni mpya ili kuliepusha taifa na machafuko ambayo
yanaweza kutokana na mizengwe ambayo ilijitokeza wakati wa uchaguzi wa
Serikali za Mitaa?” alihoji Mbowe.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Pinda alianza kwa kukubaliana na
Mbowe kwamba mchakato huo umekuwa na matatizo makubwa kifedha ingawa kwa
saa Serikali tayari imepata fedha na iko tayari kutekeleza mpango huo
wa kuandikisha wapigakura kwenye daftari la kudumu.
Alisema kuwa Serikali imekuwa ikilifanyia kazi suala hilo kwa bidii
kubwa ili kuhakikisha kuwa lengo la kuandikisha wapigakura kwenye
daftari la kudumu linatimia.
“Ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbowe ni kwamba ratiba
tuliyopewa na Tume ili kuwezesha mchakato huo kukamilika na zoezi lile
kufikia tamati likiwa katika hali nzuri na kuwahakikishia Watanzania
kwamba zoezi limefanyika vizuri, ndiyo sasa hivi inayotuongoza, kwa hiyo
tunaamini kabisa kwa ratiba hiyo waliyotupa, na sisi tumeshaanza
kudepost funds ili kuhakikisha tunakoenda na phase wanayoitaka,
kulingana na mpango walivyouweka wao wenyewe, mimi naamini zoezi hili
litakamalika kama Tume inavyotaka,” alisema Pinda.
Alisema kuwa kinachohitajika hivi sasa ni lazima kuwapo na
ushirikishwaji wa wadau wote hasa viongozi wa vyama vya siasa ili
kufikia makubaliano ya utekelezaji wa malengo hayo.
“Tunachoomba sasa ni Tume kukaa na viongozi wa vyama vya siasa
katika kila hatua ili waweze kuakikishiwa kuwa ni namna gani mchakato
unavyokwenda, tukifanya hili nadhani linaweza likatupa comfort kubwa,”
alisema Pinda.
Aidha Pinda alisema kuwa vifaa vya BVR 250 vilivyoletwa nchini
vilikuwa ni kwajili ya kupima uwezo wake ili kuwa na uhakika kwamba
havitaleta mgogoro wakati wa utendaji.
Alisema kuwa baada ya vifaa hivyo kuwasili, Serikali iliwataka
watengenezaji wa vifaa hivyo waje nchini na walikuja kwa ajili ya
kushiriki majaribio ya vifaa hivyo.
Pinda alikiri kuwa ni kweli kulibainika matatizo ya hapa na pale
ya kitaalam ambayo waliwataka wayarekebishe ili vifaa hivyo viweze
kufanya kazi kwa ufanisi.
“Lakini kwa sehemu kubwa vifaa vile vilionekana uwezo wake na
capacity yake, yaani uwezo wake wa kuandikisha Watanzania kwa siku ni
mara mbili ya kile tulichokuwa tumefikiria hapo awali, kwa maelezo haya
ni imani yangu kwamba zoezi litakwenda vizuri kwa muda unaotakiwa na
tulitumia daftari hilo katika kura ya maoni na baadaye kwenye uchaguzi
mkuu,” alisema Pinda.
Katika swali lake la nyongeza, Mbowe alisema kuwa kuanzia sasa
zimebaki siku 90 kuelekea kwenye kura ya maoni na kwamba wanasiasa siyo
wataalam wa masuala ya IT, na walitegemea kuwa wadau wangeshirikishwa
kuanzia namna ambavyo mfumo huo unavyofanya kazi, lakini inavyoonyesha
ni kwamba Serikali inajua na kama Serikali inajua maana yake ni kwamba
Chama Cha Mapinduzi kinajua hali ambayo inaonyesha kuwa wapinzani
hawatashirikishwa vya kutosha.
Aidha, Mbowe alisema kuwa katika majaribio imeonyesha kuwa vifaa
hivyo vinao uwezo wa kuandikisha watu 22 kwa siku na kwamba kutokana na
idadi kubwa ya Watanzania wenye sifa ya kuandikishwa muda hautatosha.
Mbowe alimtaka Waziri Mkuu kuutangazia umma wa Watanzania kwamba
Tume itatoa muda wa kutosha wa kujiandikisha badala ya kutumia utaratibu
wa haraka haraka aliouita ‘Vodafasta’ ili wananchi wapate haki yao ya
msingi ya kupiga kura.
Mbowe alisema hata watu wanaotarajiwa kutumika kuandikisha
wapigakura, baadhi yao ni watumishi wa Serikali ambao wengi wao hawana
uelewa wa IT, hivyo akapendekeza zoezi la kura ya maoni liahirishwe.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema kuwa anaheshimu mawazo ya Mbowe
na asingependa kubishana naye huku akisema kuwa anachosema kinatokana na
maelezo aliyopewa na Tume, lakini akasema kuwa ikiwa itabainika kwamba
suala hilo haliwezekani atarejea tena bungeni na kueleza.
Hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa, wananzuoni, viongozi wa dini na
wadau mbalimbali wamekuwa wakiishauri Serikali kuahirisha zoezi la
kupiga kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa hadi baada ya uchaguzi
mkuu wa mwaka huu kwa madai kuwa hakuna maandalizi ya kutosha.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba, alisema kuwa suala la kupiga kura ya maoni Aprili 30, mwaka huu
ni ndoto kutokana na kusuasua kwa maandalizi ya suala hilo, huku kukiwa
hakuna mikakati yoyote iliyofanyika ya kuwapatia wananchi elimu.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment