Dar es Salaam. Ujumbe maalumu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa) umetua nchini kwa siri kuchunguza tuhuma za upangaji matokeo
unaowakabili waamuzi watatu waliosimamishwa tangu mwaka jana.
Waamuzi hao, Jesse Erasmos, Hamis Chang’walu na
Oden Mbaga ambao awali walikuwa na beji ya Fifa, walisimamishwa kwa
tuhuma ambazo hazijawekwa wazi.
Julai 24 mwaka jana, Rais wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alitangaza kuwasimamisha waamuzi
hao kwa tuhuma za kupanga matokeo, ambazo hakuziweka wazi.
“Waamuzi hao waliosimamishwa na TFF pamoja na watu
wengine watahojiwa na ujumbe huo wa Fifa na matokeo ya uchunguzi huo,
yatatangazwa na Fifa wenyewe baada ya shughuli hiyo kukamilika,” alisema
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura.
“Tunaendelea kuwahimiza wanafamilia wa mpira wa
miguu nchini wazidi kuzingatia kanuni za maadili za TFF, Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na zile za Fifa katika utendaji wao. Fifa
kwa upande wake itahakikisha kuwa haki inatendeka katika uchunguzi ambao
inaufanya,” alisema.
Hata hivyo, akifafanua suala hilo, Katibu Mkuu wa
TFF, Celestine Mwesigwa alisema: “Mwaka jana tulipokea barua ya Fifa
ikitutaka kuwasimamisha waamuzi hao na kwamba wapo kwenye uchunguzi,
sasa huo uchunguzi hatutajua unahusisha mechi za ndani au za nje za
kimataifa au zote kwa pamoja.
“Sisi (TFF) tumewaandalia sehemu maalumu
watakayofanyia shughuli yao, lakini hakuna kiongozi yeyote anayeruhusiwa
kusikiliza hadi uchunguzi wao utakapokamilika, ndiyo watatuletea,”
alieleza Mwesigwa
Post a Comment