KAMA SIYO MUZIKI WANGEKUWA PANYA ROAD




Msanii wa Hip Hop Bongo, Kala Jeremiah akipozi katika ndinga lake.
Makala: Chande Abdallah na Deogratius Mongela/Ijumaa Wikienda
WAKATI watu wengine wakikata tamaa na kutojibidiisha huku baadhi ya vijana wakijiingiza kwenye makundi ya uporaji kama Panya Road katika kuyatafuta mafanikio kupitia uwezo na vipaji walivyopewa na Mungu, wafuatao ni baadhi ya mastaa ambao kwa vipaji vyao wameweza kwa namna moja au nyingine kuvumilia msoto na hatimaye kutoka kimaisha:-
Kala Jeremiah
Akiwa jijini, Mwanza mwanzoni mwa mwaka 2002 alijiingiza kwenye biashara ya mitumba maeneo ya Mlango Mmoja. Mwaka 2005 aliingia ndani ya Jiji la Dar akiwa hana ndugu yeyote hali iliyomfanya awe anashinda studio za kurekodia muziki huku akidandia chakula na malazi kwa chipukizi wenzake. Kala alishawahi kujiingiza kwenye mchezo wa kamari kama njia pekee ya kujiingizia kipato, nyota yake ilianza kuonekana baada ya kuingia ndani ya mashindano ya Bongo Star Search (BSS) yaliyofanyika mwaka 2006 na baada ya hapo akawa staa.
Msanii wa mziki wa Bongo Fleva,Shilole.
Shilole
Akiwa Tabora, Igunga alishawahi kuuza genge na kufanya kazi ya mama n’tilie, katika maisha hayo alijikuta akibakwa na kupata ujauzito akiwa katika umri mdogo huku malezi ya mtoto wake yakimkabili. Miaka ya 2010 akiwa Dar, alipata nafasi ya kuonesha kipaji chake cha uigizaji na kufanikiwa kukubalika na kuwa staa mkubwa kabla ya kuingia kwenye muziki wa Bongo Fleva ambapo anaonekana kukubalika zaidi.Mkali wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz akipozi.
Diamond
Jina lake halisi ni Nasibu Abdul, jamaa anatajwa kati ya mastaa ‘waliohustle’ mbaya ambapo akiwa anaishi maeneo ya Tandale, jijini, Dar.  Aliwahi kuuza mitumba baadaye alihamia kwenye kiwanda cha kutengenezea mabegi kilichopo Mikocheni kwa mshahara mdogo ambao sawa na bure na baadaye alijishughulisha na kuuza mafuta, kabla ya kutoboa kimuziki akiwa chini ya Sharobaro Records.Msanii wa Bongo Fleva, Nay wa Mitego akipozi.
Nay wa Mitego
Jina lake kamili ni Emmanuel Elibariki. Jamaa alinukuliwa kwenye baadhi ya ‘interview’ zake kuwahi kufukuzwa nyumbani kwa wazazi wake na kuanza maisha ya kujitegemea ambapo alijiingiza kwenye kazi za saluni kama kinyozi wa deiwaka. Nay anasimulia kuwa kwa kazi hiyo aliendesha maisha yake na kulala hapohapo saluni. Baadaye akaamua kujiingiza kwenye muziki na kuanza kukubalika hatimaye kuwa staa mkubwa.

Dude
KABLA ya kuwa staa, Kulwa Kikumba ‘Dude’ Alishawahi kupitia hali ngumu ya kimaisha hadi kufikia hatua yakufanya kazi kama muhudumu wa baa kabla ya kuhamia kwenye uchomeleaji wa mageti, miaka ya 1998. Baadaye alianza harakati za sanaa na kuwika akiwa huko hadi sasa.Msanii wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper Masawe.
Wolper
Jacqueline Wolper aliingia jijini, Dar na kuanza kufanya kazi za kutembeza vyombo mitaani chini ya kampuni fulani ya mauzo. Baadaye alijiingiza kwenye masuala ya saluni. Mwaka 2009 alishawishika kujiingiza kwenye sanaa ya maigizo na kutoboa akiwa huko.

AY
kwa mujibu wa paspoti yake anaitwa Ambwene Yessaya, jamaa aliingia jijini miaka 1996 akiwa hana ndugu yeyote. Akiamini muziki utamtoa, AY anasimulia kuishi kwa kudandia nyumbani kwa rafiki yake aliyekuwa chini ya himaya ya wazazi. Baadaye aliihama nyumba hiyo baada ya wazazi wa rafiki yake kuwa na maswali mengi juu yake kuhusu wapi ametokea na wazazi wake ni akina nani! Alishawahi kulala kwenye kontena moja lililopo maeneo ya Upanga, jijini Dar na kukaa muda mrefu bila kula.
Msanii wa Bongo Fleva kitambo, 'AY' akipozi.
Pamoja na kukesha studio, alishawahi pia kutembea kwa miguu kutoka Upanga hadi Mnazi Mmoja kila siku akienda kuoga na kufua nguo zake katika vyoo vya umma vya Uwanja wa Mnazi Mmoja ambavyo enzi hizo vilikuwa bure, baadaye aliamua kujikita kwenye muziki akiwa mdogomdogo na kufanikiwa kuibukia katika Kundi la East Coast Team lililokuwa na makazi yake Upanga, jijini Dar.

Post a Comment

Previous Post Next Post