Kopunovic ampoteza Pluijm

KOCHA mpya wa Simba, raia wa Serbia, Goran Kopunovic, amemfunika vibaya kocha wa watani wao, Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, baada ya kuiongoza timu hiyo kushinda mechi zake zote tangu alipotua nchini kuchukua mikoba ya Mzambia, Patrick Phiri.
Kopunovic ambaye amejiunga na Simba hivi karibuni, ameiongoza timu hiyo katika mechi sita na zote imefanikiwa kuibuka na ushindi, jambo ambalo linamfanya amfunike vibaya Pluijm ambaye pia amejiunga na Yanga hivi karibuni akichukua mikoba ya Mbrazili, Marcio Maximo.
Mechi hizo ambazo Kopunovic ameshinda zote ni dhidi ya JKU, Mafunzo, Taifa Jang’ombe, Polisi Zanzibar, Mtibwa Sugar na Ndanda FC.
Kwa upande wa Pluijm, tangu ajiunge na Yanga, ameiongoza timu hiyo katika mechi sita kama ilivyo kwa mwenzake huyo wa Simba, lakini ameshinda mechi tatu, ametoa sare mbili na amefungwa moja.
Mechi ambazo Pluijm kaiongoza Yanga kushinda ni dhidi ya Taifa Jang’ombe, Shaba na Polisi zote za Zanzibar, wakati alizotoa sare ni dhidi ya Azam na Ruvu Shooting huku mchezo ambao timu hiyo ilichezea kichapo ni ule wa robo fainali ya Kombe la Mapinzduzi dhidi ya JKU ya Zanzibar.
Mafanikio hayo ya Kopunovic aliyoyapata katika mechi hizo sita, yamerudisha matumaini ya Wanasimba yaliyokuwa yamepotea wakati timu hiyo ilipokuwa ikifundishwa na Phiri ambapo ushindi kwake ilikuwa ni ndoto.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, ameliambia gazeti hili kuwa, anaamini timu hiyo itaendelea kufanya vizuri chini ya Kopunovic, hivyo amewataka Wanasimba wote kumpa ushirikiano kocha huyo mwenye mbwembwe nyingi anapokuwa uwanjani.
Lakini akizungumza baada ya ushindi dhidi ya Ndanda juzi Jumamosi, Kopunovic amewataka Wanasimba watulie, kwani ndiyo kwanza anaianza kazi na mambo mazuri yanakuja.
“Ninatambua upinzani uliopo ligi kuu ni zaidi ya ule wa Kombe la Mapinduzi, lakini nina kikosi kizuri, wachezaji wote wana uwezo mkubwa na wana ari ya matokeo mazuri.
“Ndiyo kwanza ninaanza kazi, kadri siku zinavyozidi kwenda mbele ndiyo kikosi kinazidi kuimarika. Timu zilizopo mbele yetu zinatakiwa zikae mkao wa tahadhari,” alichimba mkwara Kopunovic.

Post a Comment

Previous Post Next Post