Lembeli: Muhongo anaiangamiza CCM, Amtaka ang'oke kufuta hasira za wananchi

  Amtaka ang'oke kufuta hasira za wananchi
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, amemvaa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akieleza kuwa kuendelea kwake kuachwa kwenye wadhifa huo kunachochea hasira za wananchi.

Akizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki, Lembeli alisema hajaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali katika kutekeleza maazimio ya Bunge katika kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

“Huwezi kumwambia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini apumzike apishe upelelezi, bosi wake ambaye ndiye mwenye instrument unamwacha,” alisema.

Alisema: “Nafarijika kusikia kwamba process inaendelea lakini kadiri wanavyozidi kumwacha Muhongo kwenye hiyo nafasi ndio kadiri Watanzania wanazidi kuchukia, kukasirika na wanapandisha hasira na wanaichukia serikali.”

“Nakupa mfano, kuliwahi kutokea kashfa nyingi mojawapo ni ile ya Richmond, Lowassa (Edward) alipewa nafasi ya kujitetea, alipewa nafasi ya kukaa kwenye madaraka wakati uchunguzi unafanyika?” alihoji.

Edward Lowassa alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, kufuatia kashfa ya serikali kuipatia kampuni ya kufua umeme ya Richmond zabuni ya kufua umeme wa megawati 100, wakati ilikuwa bandia na haikuwa na uwezo wa kufua umeme.

Lembeli alisema katika sakata la usafirishaji wanyama hai, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, naye alijiuzulu japokuwa waliohusika kwenye sakata hilo ni maofisa wa taasisi zilizokuwa ndani ya Wizara yake.

“Sakata la Maige ambalo mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya uchunguzi, Maige hakupewa nafasi ya kujitetea, aliondoka. Operesheni tokomeza, mawaziri wanne waliondoka na hawakupewa nafasi ya kujitetea, huyu Muhongo ni nani?” alihoji Lembeli.

Alisema kwa hali ilivyo, hata kama ni msafi, angewajibika kiutendaji kwa kuwa kashfa ya Escrow inahusu wizara anayoisimamia.

 “Kuna sababu gani kuwapeleka watu mahakamani eti kuhoji namna walivyopata pesa halafu unamwacha mtu ambaye ndiyo mwenye mamlaka ya ile wizara, hakuna sababu, hawa ni vidagaa tu.”

“Muhongo apumzike ni mwana CCM mwenzangu, lakini apumzike kwa sababu rekodi yake miaka ijayo haitakuwa nzuri kwa sababu anang’ang’ania kitu ambacho kitamharibia badae,” alisema.

Alisema rais mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, anaheshimika nchini pamoja na kwamba aliwahi kujiuzulu aliokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Alisema kitendo hicho kilimjengea heshima na baadaye alikuwa Rais ambaye hadi leo anaheshima kuwa nchini.

Alisema hajaridhishwa na hatua zilizochokuliwa na serikali kwa kuwa waliopelekwa mahakamani ni vidagaa.

Waliotakiwa kuwajibishwa na ni Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco); Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na Waziri Muhongo, ambao walitakiwa kuwajibishwa na mamlaka ya  uteuzi.

Wengine ni wenyeviti wa Kamati tatu za Bunge hilo, Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Bajeti).

Bunge lilishauri kuwa hatua za haraka zichukuliwe na Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge.

Hadi sasa aliyefukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete ni  Prof. Tibaijuka na huku Jaji Werema akijiuzulu.

Maswi alisimamishwa kazi na Katibu Mkuu, Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

WALIOFIKISHWA KORTINI
Hadi sasa watumishi watano wa serikali wamefikishwa kizimbani kwa tuhuma za kupokea mgawo wa fedha za Escrow.

Vigogo wa kwanza kufikishwa mahakamani jumatano iliyoputa ni Teophil John, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na  Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Teophil walifikishwa mahakamani kwa kudai kudai na kupokea rushwa kutoka kwa James Rugemalira, Jumatano iliyopita.

Ijumaa iliyopita Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu (BoT), Julius Angello; Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Urassa na Meneja wa Misamaha ya Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kyabukoba Mutabingwa nao walifikishwa mahakamani.

Post a Comment

Previous Post Next Post