Dodoma. Mjadala kuhusu sakata la polisi kumpiga na kumtia
mbaroni Profesa Ibrahim Lipumba jana ulikuwa mkali, lakini uliweka
bayana kugongana kwa mihimili mitatu ya nchi baada ya Bunge kujadili
suala hilo wakati likiwa limeshafika mahakamani.
Mgongano huo umetokea katika kipindi kisichozidi
miezi miwili baada ya Bunge kugoma kupokea zuio la Mahakama la kujadili
kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escow na kuendelea na
mjadala ambao ulifikia maazimio ya kuwawajibisha wahusika.
Tukio lililojadiliwa jana lilitokana na Profesa
Lipumba kukamatwa Jumanne wiki hii wakati akielekea Zakhem, Mbagala
ambako alidai alikuwa akienda kutawanya wafuasi wa chama hicho baada ya
Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara wa chama hicho
ulioandaliwa kwa ajili ya kukumbuka wafuasi 22 waliouawa mwaka 2001
wakati wakiandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.
Wakati mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia
aliwasilisha hoja juzi majira ya saa 5.00 asubuhi kutaka Bunge lisitishe
shughuli zake na kujadili suala hilo aliloliita “la dharura, kwa
maslahi mapana ya Taifa”, Jeshi la Polisi lilimfikisha Profesa Lipumba
mahakamani siku hiyohiyo lakini alasiri.
Jana, baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias
Chikawe kutoa taarifa ya Serikali kuhusu tukio hilo na kuomba radhi kwa
yaliyotokea huku akiahidi uchunguzi kwa waliohusika kutumia nguvu kupita
kiasi, Spika Anne Makinda alimsimamisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju kuzungumza.
Masaju alijaribu kuzima mjadala huo kwa maelezo
kuwa tayari Profesa Lipumba ameshafunguliwa mashtaka mahakamani, hivyo
haingekuwa busara kwa Bunge kujadili suala hilo.
Kila alipojaribu kusoma vifungu vya sheria
vinavyozuia muingiliano wa mihimili mitatu ya nchi, Serikali, Bunge na
Mahakama, wabunge walipiga kelele.
Hata hivyo aliendelea kuwa Bunge linaongozwa kwa
mujibu wa Katiba na Sheria, na katika Kanuni ya 64 (1), Bunge
haliruhusiwi kujadili jambo lolote ambalo liko mahakamani.
“Mihimili mitatu ni lazima isiingiliane, jambo
hili lipo bungeni kujadiliwa kwa ajili ya kutolewa maamuzi, na lipo
mahakamani kwa ajili ya kutolewa maamuzi, lakini mahakama ndiyo
inayoweza kutoa maamuzi ya mwisho,” alisema Masaju.
“Kutokana na mazingira haya, naomba nilishauri
Bunge lisijadili jambo hili,” alisema mwanasheria huyo aliyeteuliwa
mapema mwezi huu.
Lakini baada ya kumaliza hoja zake, wabunge
walipiga kelele na baadhi wakisema wanataka muongozo. Baadaye Spika
Makinda alisema Bunge litajadili suala hilo.
Wabunge walijadili kwa kina tukio lote la kupigwa
na kukamatwa kwa Profesa Lipumba kujaribu kuonyesha kuwa kiongozi huyo
hakufanya kosa kwa kuwa chama kilifuata taratibu zote za kulitaarifu
Jeshi la Polisi na kwamba baada ya amri ya kuzuia maandamano na mkutano,
alitii amri, hoja ambazo zinaonekana kupinga mashtaka yaliyoko
mahakamani kuwa Lipumba na wafuasi 32 wa CUF waliandamana bila ya
kibali.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment