Lipumba awaponza kina Pinda, Chikawe

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Sakata la kupigwa na kudhalilishwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi wengine wa chama hicho, limeibua mapya, baada wabunge wa upinzani kuja juu wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe wawajibike au Bunge liwawajibishe.
Wengine, ambao wabunge wanataka wawajibike ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, naibu wake (DIGP), Abdukrahman Kaniki, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Paul Chagonja pamoja na wote waliohusika na kadhia hiyo.
Pia wametaka viongozi wengine wa polisi waliohusika ama kutoa amri au kutekeleza unyama huo wachukuliwe hatua za kisheria na jeshi hilo lifumuliwe na kuundwa upya.
Walisema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakichangia bungeni mjadala kuhusu hoja iliyohusu jambo la dharura, iliyotolewa na Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia na kauli ya serikali, kuhusiana na yaliyotokea Januari 27, mwaka huu, Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Katika mjadala huo, Waziri Chikawe pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, walipatwa na wakati mgumu wakijaribu ama kutoa hoja za kuzuia mjadala kuhusu suala hilo kufanyika bungeni au kuwatetea polisi na kumkandamiza Prof. Lipumba.
Kila viongozi hao walipozungumzia mambo hayo, wabunge wa upinzani walikuwa wakipaza sauti zinazoashiria kuwapinga, kuwakejeli na kuzomea.
LISSU
Wa kwanza kuchangia mjadala huo ulioruhusiwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa sharti la kutokutoa kauli zinazoingilia mhimili mwingine wa dola, alikuwa ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Lissu kwanza alikosoa kauli ya Masaju ya kulishauri Bunge liache kujadili kadhia hiyo kwa kuwa kuna kesi iko mahakamani, akisema yeye siyo mshauri wa Bunge na kwamba, kama linahitaji kushauriwa kisheria litashauriwa na katibu wa Bunge na wanasheria wake na siyo AG.
Alisema kauli ya serikali kuhusiana na madhila yaliyotendwa na askari wa Jeshi la Polisi dhidi ya Prof. Lipumba na wafuasi wengine wa CUF, iliyotolewa bungeni jana na Waziri Chikawe imejaa uwongo
Alisema kauli ya Waziri Chikawe imewapa ufahamu kuwa ile kauli iliyowahi kutolewa bungeni na Waziri Mkuu, Pinda ya kuamuru kila anayekaidi amri ya polisi kupigwa, ni ya serikali nzima, haikuwa ya bahati mbaya na pia ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Na kwa sababu ni kauli ya serikali, mtu mwingine, mbaye hapaswi kuendelea kubaki katika nafasi yake kwa dakika moja zaidi, ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,” alisema Lissu.
Alisema Jeshi la polisi limetekwa nyara na viashiria vya ufashisti, ambazo zinaungwa mkono na kubebwa na viashiria vya aina hiyo ndani ya CCM na serikali.
“Kumbe tunapigwa siyo kwa sababu tuna makosa, tunapigwa kwa sababu kuna mafashisti ndani ya polisi, kuna mafashisti ndani ya serikali, hawa ambao wamesema tupigwe tu,” alisema Lissu.
Alisema katiba ya nchi imetamka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Pia alisema sheria ya vyama vya siasa imeeleza wazi kwamba, moja ya haki za vyama hivyo ni pamoja na kufanya maandamano na mikutano ya hadhara.
"Na sheria ya Jeshi la Polisi mheshimiwa Spika anayoizungumzia huyu waziri (anamuonyesha Chikawe) asiyepaswa kuwapo hapo tena, imewapa polisi mamlaka ya ku-regulate (kudhibiti) mikutano ya hadhara na maandamano, siyo kuyapiga marufuku," alisema Lissu.
Aliongeza: "(sheria hiyo) inawaruhusu kukwambia usifanye leo (maandamano), fanya kesho, usitumie njia hii, tumia njia ile. Haiwapi mamlaka ya kukataza maandamano na mikutano ya hadhara.”
Alisema viongozi wote wa vyama vya siasa hakuna asiyekuwa na majeraha, makovu, ambaye hajakamatwa na kunyanyaswa na Jeshi la Polisi.
Lissu alisema wengi wa wanasiasa wana kesi nyingi za uwongo zilizotungwa na Jeshi la Polisi na kwamba, Watanzania wengi wameuawa na jeshi hilo.
Alisema pia aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, aliuawa na jeshi hilo kwa amri ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, ambaye amepandishwa cheo na hivi sasa yuko makao makuu ya jeshi hilo, jijini Dar es Salaam.
“Watu wetu wameuawa Arusha 2011, wakauwa Arusha 2012 na 2013, wameuawa Morogoro, wameuawa Nzega na Jeshi la Polisi. Serikali hii na jeshi lake imetekwa nyara na fashistic elements (viashiria vya ufashisti),” alisema Lissu.
Aliongeza: "Prof. Lipumba amepigwa siyo kwa sababu alikataa (kutii) amri (ya polisi), alitamka, imeonekana dunia nzima kwenye televisheni. Waziri mzima unakuja kudanganya umma hapa."
Hivyo, akasema katika mazingira, ambayo Jeshi la Polisi limetekwa nyara na viashiria vya kifashisti, serikali inasema “wapigwe tu” na jeshi hilo limebadilisha hata namba za magari yake kutoka STK kuwa PT “Piga Tu”, Bunge lazima lichukue hatua.
Pia IGP Mangu, DIGP Kaniki, Chagonja na wote wanaohusika, wawajibike.
Alisema pia yanahitajika mabadiliko makubwa ya kimfumo wa jeshi hilo na kwamba ili yapatikane, inahitajika sera na sheria za nchi zilizopo kuhusu ulinzi na usalama wa raia zitamke wazi wazi kuwa Jeshi Polisi halina mamlaka ya kuzuia maandamano wala mikutano ya hadhara.
Kutokana na hali hiyo, alisema umefika wakati wa kuwafukuza kazi wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kwenye kamati za ulinzi na usalama akisema hao ndiyo wamekuwa chanzo cha wapinzani na raia wengine kupigwa.
"(Hao) ni makada wa CCM, ni wajumbe wa vikao vyote vya CCM kwenye ngazi za wilaya, kwenye ngazi za mikoa ndiyo wanaowaamuru ma-OCD (wakuu wa polisi wilaya) watupige, ndiyo wanaowaamuru ma-RPC (makamanda wa polisi mkoa) watupige," alisema Lissu.
Alisema Tanzania haiwezi kujiita nchi ya mfumo wa vyama vingi halafu ikaendekeza mambo ya kikatili, ya kifashisti yaliyofanyika Januari 27, mwaka huu.
Alisema Watanzania hivi sasa wanaelekea kwenye uchaguzi mkuu, lakini kwa ushahidi uliokwishaonekana kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa Jeshi la Polisi kupiga watu bure, kama kelele hazitapigwa sasa, basi maafa makubwa yanawasubiri Aprili wakati wa kura ya maoni na Oktoba wakati wa uchaguzi huo.
MNYAA
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, alisema CUF ilitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu maandamano hayo tarehe 22 na siyo 26 kama ilivyoelezwa na Chikawe, bungeni.
Hata hivyo, alisema jeshi hilo halikujibu lolote hadi tarehe 27 asubuhi siku, ambayo maandamano yalipangwa kufanyika, ndiyo waliipelekea CUF barua ya kuwaarifu kuzuia mkutano wa hadhara na maandamano hayo.
Alisema polisi walifanya hivyo wakati CUF wakiwa wamekwishafanya maandalizi makubwa  gharama nyingi zikiwa zimetumika, ikiwamo kukodi redio na televisheni kwa ajili ya kurusha matangazo ya shughuli hizo.
Hata hivyo, alisema Prof. Lipumba kwa kutii amri ya polisi alikwenda Temeke Mwisho na kuanza kutoa matangazo ya kuzuia maandamano kufanyika na kuwatawanya wananchi.
Alisema kitendo cha Waziri Chikawe kwenda bungeni kueleza kitu tofauti ni jambo linalosikitisha na kutia aibu kwa Bunge, ambalo linadanganywa, huku wabunge wakipiga kimya.
Aliungana na Lissu kutaka Pinda ajiuzulu kutokana na kauli yake “wapigwe tu” vinginevyo, arudi bungeni kwenda kuifuta na pia jeshi la polisi livunjwe.
MKOSAMALI
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema hashangazwi na Jeshi la Polisi kuwatendea hayo raia, kwani ripoti ya Jumuiya ya Madola imeeleza  bayana kuwa bado lina mifumo ya wakoloni ya kuhakikisha wanabaki madarakani.
NASARI
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari, alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilipendekeza polisi wachukuliwe hatua, lakini hadi leo hakuna aliyechukuliwa hatua.
MASUDI
Mbunge wa Tumbe (CUF), Masudi, alisema Prof. Lipumba ni sawa na Rais Jakaya Kikwete, kwa kuwa wote ni wenyeviti wa vyama vya siasa, hivyo anawashangaa polisi kushindwa kumpa heshima inayostahili na kuwa Waziri Chikawe hafai kuongoza Jeshi la Polisi, hivyo akae pembeni.
SALIM
Mbunge wa Mtambile (CUF), Masudi Abdallah Salim, aliitaka serikali kueleza amri ya kumshughulikia Prof. Lipumba na wananchi inayoelezwa kuwa ilitoka juu, ni sehemu gani?
MBOWE
Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, kwa kuwa Rais na waziri mkuu wameshindwa kuchukua dhidi ya polisi wanaowafanyia madhila wananchi, iundwe kamati teule ya Bunge kushughulikia tatizo hilo.
SHEKIFU
Mbunge wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu, alisema vurugu zote zinazotokea chanzo chake ni watu kuvunja sheria na kwamba, amebaini kuwapo na njama za kutaka kulitumia Bunge kama chombo cha kubadilisha mambo, hivyo akasema kamwe hawawezi kukubali kuona amani inavunjika, badala yake watapambana.
Hata hivyo, alisema kama kuna polisi waliotumia nguvu kubwa, basi wachukuliwe hatua.
NKUMBA
Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba, alishauri wahusika wote kuchukuliwa hatua kwani hakuna mbunge anayeweza kutetea maovu.
KASSIM
Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa, aliwalaumu CUF kutaka kufanya maandamano hayo kukumbuka watu waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi visiwani Zanzibar, Januari 27, 2001, huku wakishindwa kufanya hivyo kwa askari polisi aliyechinjwa katika tukio nilo.
SADIFA
Mbunge wa Donge (CCM), Sadifa Juma Khamisi, alisema haki ya kuandamana ipo kwenye katiba, lakini haipaswi kutumiwa vibaya, kwani katiba hiyo hiyo inaeleza kuwa hakuna haki isiyokuwa na mipaka.
Kauli hiyo nusura ichafue hali ya hewa bungeni baada ya wabunge wa CUF kumjia juu kutaka kumshughulikia kabla ya Spika Makinda kuingilia kati na kumtaka afute kauli yake hiyo.
LUSINDE
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alipinga hoja ya kutaka viongozj nao kujiuzulu kwa madai kwamba, kitendo cha polisi kimeonyesha uimara ilionao serikali ya CCM, ambayo mara kwa mara wapinzani wamekuwa wakiita dhaifu.
Awali, akisoma kauli ya serikali, Waziri Chikawe alisema yaliyomkuta Prof. Lipumba, yametokana na kukaidi amri ya polisi iliyozuia kuandamana.
Wakati Chikawe akisoma kauli hiyo ya serikali, wabunge wa upinzani walikuwa wakizomea na kumwita mwongo.
Hata hivyo, alisema katika Jeshi la Polisi kuna kitengo cha malalamiko, hivyo kama kuna mtu ana malalamiko, ayawasilishe huko.
Hali ya kuzomea na kutoa maneno ya kumpinga, ilijitokeza wakati Masaju aliposimama bungeni na kulishauri Bunge kwamba, halipaswi kujadili suala hilo kwa kuwa liko mahakamani na kwamba, kufanya hivyo, ni kukiuka katiba ya nchi.
Hata hivyo, Spika Makinda aliamua mjadala huo uendelee, lakini wachangiaji wajiepushe kutoa kauli zinazoingilia mihimili mingine ya dola.
WAFUASI 29 WA CUF KORTINI
Katika hatua nyingi, Shabani Ngurangwa na wenzake 29, ambao ni wafuasi wa CUF, jana walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya Jeshi la Polisi nchini.
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emmilius Mchauru.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, akisaidiana na Hellen Moshi, ulidai kuwa Januari 27, mwaka huu eneo la Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la jinai.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza katika ofisi ya CUF, iliyopo karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke, jijini, washtakiwa walifanya mkusanyiko usio halali kwa nia ya kufanya maandamano kwenda Mbagala.
Maugo alisema katika shitaka la tatu kuwa, siku ya tukio la pili washtakiwa bila kujali tangazo lililotolewa na jeshi hilo la kuzuia wasifanye maandamano hayo, lakini walikaidi na kufanya maandamano kwenda Zakhem Mbagala.
Mbali na Ngurangwa, washtakiwa wengine ni, Shabani Tano maarufu kama kasakwa (29), shabani Polomo (40), Juma Matar (54), Mohamed Kirungi (40), Athuman Ngumwai (40), Shaweji Mohamed (39), Abdul Juma (40), Hassan Said (37), Hemed John (49), Mohamed Ibrahim (31), Issa Hassan (53) na Allan Ally (53).
Wengine ni, Kaisi Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Alawi Msenga (53), Mohamed Matutuma (33), Salehe Ally (43), Abdul Hatibu (34), Bakari Maliya (43)Abdallah Ally (32), Said Mohamed (40), Salima Mwafisi, Salehe Rashid (25), Abdallah Said (45), Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athumani Said (39), Dickson Lesson (37) na Nurdin Msati (37).
Washtakiwa wote walikana mashitaka hayo. Hakimu Mchauru alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana kwa kusaini hati ya dhamana ya Sh. 100,000 kila mmoja na mdhamini mmoja atakayesaini kiasi hicho cha fedha.
Washtakiwa wamepelekwa mahabusu hadi leo kesi hiyo itakaposikilizwa dhamana yao.
CUF WALAANI
Wakati huo huo, CUF kimelaani  vikali  Jeshi la Polisi nchini kumkamata, kumdhalilisha  na kumpiga Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, pamoja na wafuasi wake katika vurugu zilizotokea Januari 27 baina ya jeshi la polisi na wafuasi wa chama hicho.
Pia kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha viongozi wote ambao kwa namna moja ama nyingine walihusika katika tukio hilo.
 Makamu Mwenyekiti CUF Taifa, Juma Duni Haji, alisema Jeshi la Polisi linatekeleza vitendo hivyo kutokana na mashinikizo ya kisiasa.
Haji alisema ni jambo la kushangaza kuona jeshi hilo linashindwa kutumia nguvu kulinda usalama katika maandamano, lakini linatumia nguvu kubwa kupambana na kupiga raia wasio na silaha.
Alisema ni vema rais akaliangalia na kulishughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira sawa ya ushindani wa kisiasa, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu ili kuepuka kuiingiza nchi katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Kadhalika, aliongeza kuwa CUF kitaendelea na msimamo wake wa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi na kuwakumbuka wenzao waliojitoa mhanga kwa ukombozi wa kidemokrasia nchini.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post