NI KOSA LENU WADADA, SIYO WANAUME!

MAISHA yanakimbia kuliko treni iendayo kasi. Sasa hivi kama mtu akija na kukuambia habari za mwaka mpya, anasema hivyo kwa mazoea tu, lakini ukweli halisi ni kwamba mwaka umeshakomaa huu, watu wameshasahau kama wiki chache zilizopita, dunia  nzima ilikuwa ikizizima kwa nyimbo za Happy New Year!
Yaaa, mwaka umeshakuwa wa zamani maana hata machungu ya wazazi na walezi kwa ada walizotoa kwa wategemezi wao zimeshaisha uchungu wake.
Katika uandishi wa safu hii, nakutana na watu wengi, hasa akinadada wanaolalamika kuhusu kuumizwa na wenza wao. Na siyo tu kuumizwa, lakini pia wamekuwa wakiniuliza maswali mengine hadi unacheka, kama kutaka kujua endapo wanapendwa kweli au la na wale wanaowaamini.
Kwa kuwa inaonekana tatizo hili lipo kwa wengi, nimeona ni jambo zuri kama nitajaribu kuwasiliana na wote katika ukurasa huu, nikiwapa ujumbe kuwa katika malalamiko mengi, kama siyo yote, ambayo wanawake/wasichana wanalalamika kuhusu wenza wao, basi wao wenyewe ndiyo msingi wa matatizo yenyewe.
Hebu fikiri kwa mfano utamjibu nini msomaji anayekuuliza swali kama hili; Nina mkaka ninampenda sana, ila tatizo kila nikimtumia meseji hajibu, naomba ushauri nifanyaje?
Lakini pia kuna maswali kama wale wanaotaka kujua wenza wao wenye hasira, ambao kwao suluhisho ni kuwapiga, walevi, wanaowachukia wazazi, ndugu au walezi wao na aina mbalimbali za watu wanaodhani wana dosari!
Kama nilivyosema hapo awali, kutokana na aina ya maswali haya kuwa mengi na yanayofanana, ninaomba niwajibu kwa pamoja kuwa chanzo cha haya yote ni sisi wenyewe wadada na wala hata siyo makosa ya hao wanaume. Lakini pia kwa akina baba wenye kilio cha aina hii, kosa siyo la wanawake wao, bali ni lao wenyewe. Nitafafanua.
Katika uhusiano wa kimapenzi tunaoujenga, sisi ndiyo wahusika wakuu. Tunajijua tulivyo, kwamba hatupendi hiki, tunapenda kile na tunakwazwa na vitu vya namna hii, tunafurahia vya dizaini hii, uongo?
Sasa inakuaje unaanza kulalamika kuhusu mtu ambaye ni wewe ndiye mwenye mamlaka ya kumruhusu kuumiliki mwili na moyo wako? Binafsi, siamini katika wale wanaodai eti wamewapenda wenza wao kuliko kawaida, kwamba eti hawawezi kujinasua kutoka kwao!
Ni uongo na kujitesa bila sababu ya msingi. Yaani mimi mke au demu wangu atanitesaje? Kama nilimfuata mwenyewe, nikamwaga sera zangu, akanielewa, leo inakuaje?
Ni sawa na wewe mdada; nimekufuata nikatangaza nia, ukanisikiliza, ukanitazama juu ukanishusha, halafu ukanielewa, kinachokutesa ni nini sasa?
Ni hivi, malalamiko yetu ya leo maana yake ni kuwa jana hatukufikiri vizuri, kwamba tulikurupuka kutoa maamuzi, huenda kwa sababu tulibabaika na jinsi jamaa alivyotuingia, au tulifanya hivyo kwa kuiga au kwa namna yoyote ambayo haikuishirikisha nafsi yetu kwa nafasi inayostahili.
Niwashauri kitu, mapenzi ni kitu cha ajabu, hata siku moja tusikifanyie majaribio. Amua kwa dhati, kama unataka kuwa na huyu kwa sababu tu ya kukidhi haja yako ya kingono, fanya hivyo, lakini kama unaamini katika mtu ambaye atakuwa sehemu ya mwili wako, usikurupuke. Jiulize maswali mengi kadiri unavyoweza na lazima ujipatie majibu ya kukuridhisha!

Post a Comment

Previous Post Next Post