NINGEKUWA MIMI PROFESA LIPUMBA, NINGEENDELEA NA HARAKATI

Profesa Ibrahim Haruna Lipumba.
Kwako Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, mwenyekiti wa taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF).
Najua bado unaendelea kuuguza majeraha kutokana na kipigo kikali ulichoshushiwa na polisi siku chache zilizopita pale ulipojaribu kwenda kuwatawanya wafuasi wa chama chako waliotaka kuandamana na kuhudhuria mkutano wako wa hadhara.
Najua bado unakabiliwa na kesi ya kuwashawishi wafuasi wako kutenda kosa la jinai kwa hiyo itakuwa vigumu kwa mimi na wewe kukutana ndiyo maana nimeamua kutumia ukurasa huu kufikisha ujumbe wangu kwako.
Profesa, mimi sikuzaliwa Juni 6, 1952  Ilolangulu, Tabora kama wewe. Sikusomea Shule ya Msingi ya Swedish Free Mission kuanzia mwaka 1959 hadi 1962 na baadaye kuhamia Shule ya Msingi ya L.A Upper mwaka 1962 hadi 1966 kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tabora Boys kisha Sekondari ya Pugu na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1972 kama wewe.
Mimi sikusomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata shahada ya kwanza na ya uzamili (masters degree) kwenye masuala ya uchumi kama wewe. Sijawahi kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Stanford na kupata shahada ya uzamivu (PhD) mwaka 1983 kama wewe.
Mimi si mchumi mkubwa duniani kama ulivyo wewe, sijui chochote kuhusu mambo ya uchumi wala sijawahi kufundisha chuo kikuu mahali popote duniani kama wewe. Kichwani hamna kitu kabisa, niponipo tu mjini naungaunga.
Hata hivyo, licha ya umbumbumbu wangu, ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, walahi nakuapia nisingekatishwa tamaa wala kuvunjwa moyo na kipigo kikali cha polisi kama ulichokipata wewe pale Mtoni Mtongani, Dar, ningeendelea na harakati za kuhakikisha haki sawa kwa wote na maendeleo ya kila Mtanzania vinapatikana.
Kuandamana ni haki ya kimsingi kwa kila Mtanzania, wewe na wafuasi wa chama chako mlipoamua kuandamana ili kuwakumbuka Watanzania 22 waliopigwa na kuuawa na polisi Januari 26 na 27, 2001 kisiwani Pemba, mlikuwa mkiitumia vyema haki yenu ya kikatiba.
Ili kupata ulinzi, ulifuata sheria kwa kuwataarifu polisi kwa maandishi kwamba kutakuwa na maandamano hayo ya amani ambayo mlipanga yaanzie Temeke Mwisho na kuishia Mbagala Zakhem lakini ikadaiwa kuwa barua yenu ilikataliwa dakika za mwisho.Kilichokutokea wewe na wenzako, ndiyo picha halisi ya jinsi jeshi la polisi la nchi hii linavyofanya kazi. Badala ya kulinda usalama wa raia na mali zao, limegeuka na kuwa chombo cha kuwatesa, kuwapiga na wakati mwingine kuwaua wananchi.
Wao wenyewe hawawezi kujilinda tena ndiyo maana vituo vyao vinavamiwa kila kukicha, wanachojua ni kuzuia maandamano tu. Hata kupambana na changamoto ndogondogo za kiusalama kama wimbi la Panya Road lililozua kizaazaa jijini Dar es Salaam wiki kadhaa zilizopita, zinawashinda kabisa.
Wahenga wanasema hakuna marefu yasiyo na mwisho, ipo siku polisi watatambua kwamba nguvu ya umma ni kubwa kuliko wanavyofikiri. Nikutie moyo profesa, kilichokutokea na wenzako ndicho kinachowatokea mamilioni ya Watanzania ambao kila kukicha wanaumizwa au kuuawa na polisi, bila sababu za msingi.
Usikate tamaa ya kuendelea kuwahamasisha Watanzania kudai haki zao za msingi, endelea na harakati kwani ni bora kufa ukiwa umesimama kuliko kuishi ukiwa umepiga magoti.
Wasalaam

Post a Comment

Previous Post Next Post