IKULU imewataka Watanzania kuwa na subira kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia sasa atatoa uamuzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Muhongo na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali wanahusishwa
na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow.
Viongozi wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi
ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye amejiuzulu na aliyekuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye
tayari uteuzi wake umetenguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema si kweli Rais
Kikwete anakwepa kumwajibisha Profesa Muhongo kama watu wengi
wanavyodai.
Alisema kinachofanywa na Rais Kikwete ni kufuata utaratibu unaotakiwa.
“Siku mbili tatu alizosema rais maana yake ni hivi karibuni na msidhani
anakimbia kutoa uamuzi… siku si lazima zihesabike, ni siku yoyote atatoa
majibu.
“Tena nawaambia msikomalie suala hili kama vile ni la kufa na kupona, rais atalifanyia kazi muda si mrefu,” alisema Salva.
Alisema taratibu za kumwajibisha Profesa Muhongo kama kiongozi wa
kisiasa hazifanani na hatua zilizochukuliwa kwa Katibu Mkuu wa wizara
hiyo, Maswi kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Serikali.
Akizungumzia ziara za Profesa Muhongo anazoendelea nazo mikoani,
Rweyemamu alisema tuhuma hizo hazimzuii kufanya kazi kwa kuwa bado
hajaondolewa kwenye nafasi ya uwaziri aliyonayo.
“Huyu bado ni waziri, ana haki ya kuendelea na ziara zake kama kawaida,
kumbukeni wizara yake ina mambo mengi ambayo yanapaswa kusimamiwa kila
siku,” alisema Rweyemamu.
Desemba 22, mwaka jana, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar
es Salaam, alisema amemuweka kiporo Profesa Muhongo maana bado hajapata
ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha, na kwamba baada ya siku mbili,
tatu, atakapopata ufafanuzi na kujiridhisha, atachukua uamuzi.
Siku nne baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alinukuliwa
na vyombo vya habari akisema Rais Kikwete bado hajakamilisha
kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi
watajulishwa hatua alizochukua.
MISAMAHA YA KODI
Kuhusu misamaha ya kodi ambayo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), imesema imeongezeka kutoka Sh trilioni 1.48 mwaka 2012/13 hadi
trilioni 1.82 mwaka 2013/14, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 334,
Rweyemamu alisema wabunge ndio wanapaswa kulalamikiwa.
Alisema katika Bunge lililopita Serikali ilipeleka muswada wa kufuta misamaha ya kodi, lakini wabunge hawakuupitisha.
Rweyemamu alisema bila kupitisha muswada huo na hatimaye uwe sheria, suala hilo halitakwisha.
“Wabunge wanapiga kelele kuhusu misamaha ya kodi wakati mwaka jana
Serikali ilipeleka muswada wa kufuta misamaha waliukataa na
kuuchanachana…tunawaomba siku nyingine wakipelekewa waupitishe.
“Sisi hatupendi haya mambo na kama wanaonekana hawapendi, tunawashauri
waupitishe ule muswada ili tuondokane na tatizo hili,” alisema Rweyemamu
KURA YA MAONI
Katika hatua nyingine, Rweyemamu alikanusha taarifa zinazoendelea
kusambazwa kuwa Rais Kikwete alivunja sheria ya kura ya maoni kutokana
na kutopelekwa Katiba iliyopendekezwa kwenye Gazeti la Serikali.
“Hizi taarifa si za kweli, Rais Kikwete alitimiza taratibu zote
kulingana na matakwa ya kura ya maoni, baada ya kupokea Katiba
inayopendekezwa Oktoba 8, mwaka jana, ilipofika Oktoba 10, ilitangazwa
katika Gazeti la Serikali,” alisema Rweyemamu.
Alisema hawana hofu kwa vile maandalizi ya kura ya maoni yanaendelea vizuri.
Post a Comment