Ofisi
ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
imepeleka suala la mchakato wa uuzaji wa hisa za Halmashauri ya jiji la
Dar es Salaam katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam(UDA) kwa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kuangalia mchakato mzima
na mkanganyiko katika uuzwaji wa hisa hizo.
Pia
wamemtaka mwanasheria mkuu wa serikali kuupitia mchakato mzima kubaini
kama hisa hizo zimeuzwa kwa kampuni ya Simon Group au hazijauzwa.
Akijibu
hoja za kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
kuhusu mikataba yenye maslahi duni kwa halmashauri, Waziri wa Tamisemi,
Hawa Ghasia (pichani hapo chini) alisema kupelekwa kwa suala hilo
Takukuru pamoja na kwa mwanasheria mkuu wa serikali, ni kutaka kubaini
kama hisa hizo ziliuzwa au la na kama ziliuzwa ilikuwa kihalali?
“Suala
hili la UDA tumeamua kulipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali na
Takukuru kujua uhalali wa mchakato mzima wa uwekezaji na iwapo mauzo ya
hisa za jiji yaliuzwa kihalali au la?,” alisema.
Awali,
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya LAAC, Rajab Mbaruk Mohamed akiwasilisha
taarifa yake ya hesabu za serikali za mitaa kwa mwaka wa fedha ulioishia
Juni 30, mwaka 2013,alitaka serikali kueleza ukweli kama hisa za jiji
katika UDA zimeuzwa na kuhamishiwa kwa mwekezaji huyo au hazijauzwa.
Kamati
hiyo ilisema endapo hisa hizo hazijauzwa, mchakato wa uuzaji wa hisa
hizo utapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazohusika.
Lakini
wakati mijadala inaanza, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alipotaka
kujadili suala hilo la UDA, Spika wa Bunge Anne Makinda alimzuia na
kueleza kuwa hairuhusiwi kulijadili kutokana na kuwa serikali
walimpelekea taarifa ya kuwepo kwa kesi mbili zinazohusu UDA, hivyo
kujadili watakuwa wameingilia uhuru wa Mahakama.
Uamuzi
huo uliungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa serikali, George Masaju
aliyesema hata yeye anayo mashauri matatu ya UDA mahakamani hivyo kwa
utaratibu wa kuheshimu mihimili mingine ni vema suala la UDA
lisijadiliwe.
Akizungumzia
suala la Halmashauri ya Kinondoni kutonufaika na uwekezaji wa kampuni
ya Oysterbay Villas, alisema ukwamishaji wa Kinondoni ulitokana na
mkataba waliokubaliana lakini baada ya wiki moja Halmashauri ya
Kinondoni itaanza kunufaika na uwekezaji huo ulioanza mwaka 2010.
Ghasia
alisema ili kuondokana na mikataba yenye utata katika Halmashauri,
imeamuliwa mikataba yote kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kujua
kama mikataba hiyo ina manufaa hivyo malalamiko hayo hayatarudia.
Post a Comment