LEO tunaimaliza rasmi Januari, kwa
sababu watakaobahatika kuamka salama kesho, watakuwa katika mwezi
mwingine ambao unathibitisha kwamba mwaka 2015 umeanza kukatika.
Binafsi, bado ninakumbuka siku ile ya Desemba 31, 2014 nilipolazimika kusubiri hadi saa sita na dakika moja usiku ili nipige yowe la kumshukuru Mungu kwa kuuaga vizuri.
Binafsi, bado ninakumbuka siku ile ya Desemba 31, 2014 nilipolazimika kusubiri hadi saa sita na dakika moja usiku ili nipige yowe la kumshukuru Mungu kwa kuuaga vizuri.
Tofauti na miaka iliyotangulia, huu utakuwa wa kipekee kutokana na
matukio muhimu yanayouhusu; kwanza ni upigaji wa kura ya maoni kuhusu
katiba mpya inayopendekezwa na baadaye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani. Haya ni mambo ya kuzingatiwa sana kwa sababu hayana vyama vya
siasa, ni ishu ya utaifa kwa vile yote yana uhusiano wa karibu sana na
maisha yetu ya kila siku.
Leo nina mada mezani ambayo ni mjadala wa muda mrefu katika jamii
yetu, ingawa kwa bahati mbaya sana, umekuwa hauwahusishi wahusika, kwa
maana ya wanafunzi wenyewe ili nao watoe mawazo yao. Zipo hizi kelele
zinazopigwa kuhusu lugha gani hasa inafaa kutumiwa katika masomo kwenye
shule zetu, hasa kuanzia msingi hadi sekondari.
Watu wa kisasa wanapigia debe kutumika kwa lugha ya Kiingereza,
wakiwa na hoja nzuri kabisa kuwa ni vyema tukaitumia hii kwa sababu
inatambulika na kutumika kimataifa, wakati watu wa aina yangu, bado
wanaamini katika kutumia Kiswahili, kwani licha ya kueleweka vizuri
miongoni mwa Watanzania wote, pia ni mojawapo ya njia za kuipromoti ili
nayo itambe duniani.
Ipo kasumba miongoni mwetu ya kuamini kuwa mtu anayezungumza
Kiingereza ni msomi. Ndiyo maana hata leo, wazazi wanaowapeleka watoto
wao katika shule za Academy, wakiwasikia wanazungumza maneno mawili
matatu ya Kiingereza, wanaamini vijana wao wana akili, wanashangilia na
kutembea kifua mbele. Kitu ambacho tunashindwa kuelewana baina ya
makundi haya, kiasi cha mimi kuomba uhusika wa wanafunzi, ni uelewa wa
tunachobishania. Wanaoshabikia umombo wana hoja za lugha ya kimataifa,
wakati wamatumbi tunamaanisha kuelewa kinachofundishwa.
Sipingi Kiingereza, lakini je, vijana wetu wanaelewa masomo
wanayofundishwa? Hofu yangu ni kuwa mwisho wa siku tutakuwa na vijana
wengi wanaojua ung’eng’e lakini vichwa vyao vikiwa vitupu katika ufahamu
wa mambo. Kwa nini kwa mfano, kijana wa Mikumi afundishwe kwa
Kiingereza juu ya mbuga za wanyama zinazomzunguka wakati angeelewa
vizuri zaidi kama ungetumia lugha ya taifa?
Vipo vitu vya kujifunza kwa lugha za watu, lakini upo umuhimu mkubwa
wa kuenzi lugha yetu. Tunatakiwa kufundishwa masomo ili tuyaelewe,
baadaye lugha hizi za kibiashara zifuate. Wachina hawajawahi kuipa
kipaumbele lugha yoyote nje ya kikwao, lakini wanakamata nafasi za juu
katika mambo mengi duniani, yakiwemo ya kiuchumi, kijeshi na maendeleo
ya viwanda.
Leo hii, unalazimika kwanza kujifunza lugha za Kichina ili uweze
kushughulika nao vizuri, vinginevyo itakula kwako. Lakini hili
halijawazuia Wachina kujifunza Kiingereza wala lugha nyingine za
kimataifa. Ninajua, kasumba na historia itatukataza kuepuka matumizi ya
umombo katika shule zetu, lakini upo ulazima mkubwa sana wa kuhakikisha
lugha hii inapata kipaumbele cha kufundishwa mashuleni, ikibidi zaidi
kuliko ilivyo kwa Kiingereza.
Hii ni kwa sababu ukiondoa somo la Kiswahili kama somo darasani,
katika shule hizi za Academy, hakuna somo lingine linalofundishwa kwa
lugha hii, wakati upo ukweli kuwa Kiswahili kinachotumika mitaani na
mashuleni, kina makosa mengi ya kisarufi na maana tofauti na ilivyo!
Post a Comment