Viongozi CC waliotelekeza wapigakura watoswe - Nape

Katibu wa Itikadi na Uenenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye.
Katibu wa Itikadi na Uenenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amewataka wanachama wa CCM Zanzibar kutowachagua viongozi wa CCM  katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambao walichaguliwa katika uchaguzi wa mwaka 2010, lakini  wanapuuza kuwatembelea na kukutana na  wapiga kura wao.
Aliyasema hayo wakati akiwahutubia mamia ya wananchi na wanachama wa CCM katika mkutano wa hadhara liofanyika visiwani hapa, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kuimarisha Chama Zanzibar.

Nape alisema viongozi wa aina hiyo hawakitakii meme CCM na kuwasihi wananchi kuwanyima kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Aliwataka viongozi wa CCM kuiga mfano wa raisi wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kukutana na wanachama wa CCM.

Alisema Kupitia kamati kuu ya CCM, viongozi wote wa Chama hicho wanatakiwa kutoka maofisini kwenda  kuonana na wanachama na wanapokwenda huko kuachana na itifaki ndefu kwani zinakiumiza chama na wanachama wake.

”Wengi wenu wakati mnapewa madaraka ya chama mlikuwa watu wa kawaida mkishapewa mnapandisha mabega (majivuno), sio sahihi tokeni maofini nendeni mkaonane na wanachama, ndipo namna nzuri ya kukijenga chama, mnamuona Katibu mkuu wetu Kinana anavyokaa chini na kula na mabalozi wa chama hiki,” alisema Nape.

Alimpongeza Rais Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa ziara zake za kuonana na wanachama wa CCM kwani utaratibu huo ni mzuri na umepongezwa sana na Kamati Kuu ya CCM na kluongeza kuwa na ziara hizo zinalengo la kukijenga Chama hicho na hizo ziara zimewaumiza sana Chama cha Wananchi (CUF).

Alisema yeye ndie katibu wa itikadi hakuna mwengine katika CCM, kwani itikadi ni pamoja na tabia za wananchama na viongozi hivyo asipowaambia ukweli atakuwa anakosea na hatoitendea  haki nafasi yake hiyo.

“Natoa wito kwa viongozi wa CCM kushusha mabega (kuacha majivuno) tulipowapa  nafasi za uongozi mlikuwa wanyonge, lakini mkishapewa mmekuwa na majivuno, mkinichukia shauri yenu, lakini nimeshasema nendeni kwa wanachama, acheni kukaa maofisini,” alisisitiza Nape huku akishangiliwa na wanachama waliohudhuria katika mkutano huo.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post